NA DIRAMAKINI
MBUNIFU wa mashine kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), George Nyahende amefanikiwa kubuni mashine ya kuchakata matunda na viungo kuwa katika mfumo wa unga ili kuwasaidia wakulima kuhifadhi mazao.
Akizungumza katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Nyahende amesema mashine hiyo ni bora na ya kisasa inayomsaidia mkulima hata mjasiriamali kuchakata mazao na kuyaongezea thamani.
Amesema, mashine hiyo ina sehemu tatu ambazo kila moja ina kazi yake.Akitaja kazi zake amesema, moja ni ya kukatakata viungo au matunda tayari kwa kuyakausha kwenye mashine nyingine ndogo na baada ya hapo inaingia kwenye mashine ya kusaga kuwa unga.
"Huu ni ubunifu mpya, niliona wakulima hususani vijijini wanapata hasara ya mazao yao mfano vitunguu wanavuna wakati mwingine soko halipo vinaharibika,sasa wakitumia mashine hii wanavikausha vitunguu na kuvisaga kuwa unga na hapo unahifadhi kwa muda mrefu,"amesema Nyahende.
Aliendelea kueleza kuwa, ameamua kubuni mashine hiyo kwa sababu hivi sasa maeneo mengi ya vijijini umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA),wamesambaza umeme maeneo mengi hivyo wakulima wengi wanaweza kununua mashine hiyo na kuondokana na umaskini.
Aidha, kuwa mashine hiyo sio tu kwa mkulima bali pia kwa wajasiriamali wadogo wanaweza kufungua kiwanda kidogo.
"Mjasiriamali mdogo pia anaweza kuwa na mashine hii nyumbani na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kukuza uchumi wao,"amesema.
Akizungumzia kuhusu mashine hiyo amesema, moja ya mashine hizo ambayo ni ya kukausha matunda,viungo au nyama hutumia muda kati ya saa sita hadi 12 kulingana na bidhaa na baada ya hapo unasaga na kupata unga kisha unaweza kuufungasha kwa ajili ya kuhifadhi.