NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof.Sospeter Muhongo amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kushiriki kikamilifu kuhesabiwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo itafanyika Agosti 23,mwaka huu.
Prof. Muhongo amesema, lengo la Sensa ya Watu na Makazi ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, kijamii, kiuchumi na hali ya mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali za elimu, afya, hali ya ajira, miundombinu kama barabara, nishati na maji safi.
Amesema kuwa, kwa msingi huo sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake analazimika kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa na mafanikio makubwa katika kuisaidia Serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu wa eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa utoaji wa maendeleo kwa kila eneo la utawala hapa nchini.
Ameyasema hayo leo Julai 30, 2022 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji na uelimishaji jamii juu ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Busekera katika Kata ya Bukumi Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini, chama pamoja na wananchi.
"Tunataka tuhesabiwe kwa asilimia 100, ninawaomba sana ndugu zangu tarehe 23, Agosti mkahesabiwe msiogope chochote, Serikali inataka ipate idadi ya wananchi iweze kupanga mipambo mbalimbali ya maendeleo mtaulizwa maswali una watoto wangapi?,unafanya kazi gani?, nawaomba sana mtoe ushirikiano wenu wa dhati ili Jimbo la Musoma Vijijini liweze kupiga hatua kutokana na fedha zitakazokuwa zikitolewa na Serikali kufanya maendeleo," amesema Prof. Muhongo.
"Musoma vijini tuna shule 111 za msingi, shule shikizi 5, sekondari 21, tunajenga shule nyingine 10 na maabara zinajengwa sekondari zote. Tunayo High School moja tu nimepeleka maombi serikalini naulizwa tunataka high school tuko wangapi? Nashindwa kutoa takwimu sahihi, niwaombe wananchi kusudi serikali iendelee kupanga mipango ya maendeleo na kutuletea maendeleo kwa usahihi sote tuhesabiwe siku ya sensa ili tutambulike. Mwambie ndugu yako aliyeko nyumbani ahesabiwe kwa faida yake na jimbo letu," amesema Prof. Muhongo.
Aidha, Prof.Muhongo amewataka wananchi wa jimbo hilo kutowaficha ndani watu wenye ulemavu badala yake wahesabiwe siku ya sensa. Huku akisema atapita kila kijiji kufanya hamasa na kutoa elimu juu ya umuhimu wa sensa ili watu wote ndani ya jimbo hilo wahesabiwe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule amesema kuwa, iwapo mkuu wa kaya hatakuwepo aache taarifa sahihi za watu wote katika kaya kwa mtu mzima aliyepo kusudi karani wa sensa na Mwenyekiti au kiongozi wa mtaa au kitongoji afikapo wapewe taarifa zote zinazohitajika.
"Watauliza pia kiwango chako cha elimu, shughuli zako, taarifa za ulemavu, hali ya uzazi, taarifa za umiliki wa ardhi, taarifa za vifo na vifo vitokanavyo na uzazi, hali ya nyumba, anwani za Makazi, taarifa kuhusu Mpango wa TASAF, umri, jinsi, hali ya ndoa, taarifa za uhamiaji, taarifa za vitambulisho vya taifa na uhai wa Wazazi, taarifa za majengo niwaombe toeni taarifa kwa ushirikiano wa dhati kufanikisha Jambo hilo muhimu kwa nchi yetu,"amesema Dkt.Haule.
"Kujibu maswali ya Sensa ni matakwa ya kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura namba 351. Ushirikiano wako na karani wa sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kutoa taarifa sahihi ndio utakaorahisisha na kufanikisha sensa ambapo matokeo yake yatachochea kasi ya maendeleo ya watu na Makazi yao katika maeneo yote ya utawala nchini,"amesema.
Diwani wa Kata ya Bukumi, Munubi Mussa amesema kuwa, wananchi wa kata hiyo wamejiandaa kushiriki kwa ufanisi kuhesabiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini, Bwire Nyabukika amemuomba Diwani wa Kata hiyo kuweka utaratibu mzuri ili siku ya sensa wananchi wote wahesabiwe kwani wengi wao wanajishughulisha na uvuvi.
Charles Magoma ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma ambapo amesema kuwa, maendeleo yote yanayofanywa na Serikali yanatokana na Wananchi hivyo watimize wajibu wao kuhesabiwa.