Ng'ombe 50,000 Dodoma Jiji kuvishwa hereni za kielektroniki

NA DENNIS GONDWE

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inakusudia kutambua, kusajili na kufuatilia ng’ombe 50,000 na kuwavisha hereni za kieletroniki kwa lengo la kudhibiti magonjwa na wizi wa mifugo.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga alielezea utekelezaji wa zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo na kuzivisha hereni za kieletroniki kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika katika Mtaa wa Segu chini, Kata ya Nala jijini Dodoma.

Mwesiga alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajia kutambua kwa kuwavisha hereni Ng’ombe wapatao 50,000, Mbuzi 45,000, Kondoo 10,000 na Punda 200.

Akiongelea utekelezaji wa zoezi hilo, alisema kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alitoa shilingi 33,942,000 kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo. 

“Serikali ilitoa mwongozo wa uendeshaji wa zoezi la uvishaji wa hereni za mifugo. Mwongozo huo unatoa bei elekezi ya hereni isiyozidi shilingi 1,750 kwa Ng’ombe na Punda. Shilingi 1,000 kwa Mbuzi na Kondoo,”alisema Mwesiga.

Akiongelea umuhimu wa zoezi hilo, alisema kuwa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo una faida nyingi. 

“Mifugo kutambulika mahali ilipo na umiliki wake. Udhibiti wa magonjwa yakiwemo ya mlipuko. Nyingine ni kuwa na hakikisho la usalama wa chakula na kurahisisha biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje na kudhibiti wizi wa mifugo. 

"Mwisho ni kurahisisha upatikanaji wa mifugo iliyopotea na utambuzi unawezesha urahisi wa upatikanaji wa mikopo na bina ya mifugo,”alisema Mwesiga.

Kwa upande wake, Elisha Msangi ambaye ni mfugaji alisema kuwa, zoezi hilo la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo utawahakikishia usalama wa mifugo yao. Zoezi hili litakomesha wizi wa mifugo na kuwaondolea hasara wafugaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news