NA SOPHIA FUNDI
MKUU wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Dadi Kolimba pamoja na Mkurugenzi wa halmshauri hiyo, Karia Magaro wameongoza zoezi la usafi katika mji wa Karatu na Kituo cha Afya Daboldi ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa nchini.
Akizungumza baada ya usafi huo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Karia Magaro amesema kuwa, lengo la kufanya usafi katika maeneo hayo ni kuimarisha usafi pia na kuwaenzi mashujaa waliojitoa kwa ajili ya nchi yetu.
Amewataka wananchi pale wanaposikia matangazo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wilaya kujitokeza ambapo alilaani kitendo cha wananchi kutojitokeza kwenye zoezi hilo la usafi pamoja na kutangaziwa na kuwaachia watumishi pekee yao kufanya usafi.
"Tumekuwa tukitangaza suala la usafi kwa wilaya, lakini wananchi wamekuwa hawajitokezi na kuendelea na shughuli zao na kuwaachia watumishi wakifanya usafi wa mazingira wenyewe jambo ambalo halipendezi, ninaomba tudumishe mshikamano katika kuuweka mji wa Karatu kuwa msafi ukizingatia kuwa ni mji wa utalii,"amesema Karia.
Katika kuhakikisha mji huo unakuwa msafi halmashauri imewakataza wanaopika vyakula maeneo ya mabaraza kuacha mara moja, kwani maeneo hayo yamekuwa yakijaa uchafu mara kwa mara hasa kumwangwa kwa maji machafu kwenye mitaro jambo ambalo alisema ni hatari kwa afya za walaji wa vyakula hivyo.
Amesisitiza kuwa, suala la usafi kwa kila mfanyabiashara katika eneo lake analofanyia biashara pamoja na vijiwe vya bodaboda na kila mtu awe mlinzi wa mwenzake kwa kutupa taka hivyo.
Pia amewataka wananchi kuwa na mshikamano katika kuhakikisha mji unakuwa msafi ambapo alisema hawatawavumilia wale wote wataonekana wachafuzi wa mazingira ya mji wetu.