NA SHEILA KATIKULA
UMOJA wa Makondakta na Wasaidizi wake Mkoa wa Mwanza (UVDS) umeiomba Serikali kuendelea kupunguza bei ya mafuta ili kuimarisha uchumi wa wafanyabiashara ya usafirishaji wa abiria.
Hayo amesemwa na Mwenyekiti wa Makondakta na wasaidizi wake, Mlimi Juma wakati akizungumza na DIRAMAKINI ofisini kwake.
Juma amesema, kutokana na kupanda kwa nauli kutoka shilingi 400 hadi 500 kumepelekea wakazi wa maeneo ya Mabatini na Igogo kupunguza matumizi ya kupanda gari na kutembea kwa miguu ili kuepuka gharama za usafiri.
"Wananchi wanaoishi maeneo yaliyopo karibu na mjini hawatumii usafiri wa daladala tangu nauli zilipopanda kutoka shilingi 400 na hadi 500 kitendo ambacho kinapelekea abiria kupungua na uchumi wa makondakta kushuka,"amesema.
Amesema, kutokana na changamoto hiyo mzunguko wa biashara umekuwa mdogo hali iliyopelekea makondakta kushindwa kupata fedha za kutosha kumudu gharama za uendeshaji wa magari ikiwemo upatikanaji wa hela ya mafuta,hesabu ya tajiri pamoja na posho zao hali inayosababisha ugumu wa maisha kwani wanafamilia zinazowategemea.
"Sasa hivi tupo kwenye kipindi kigumu kwa sababu biashara imekuwa na changamoto kutokana na kupungua kwa abiria kwa sababu ya ongezeko la nauli lililotokea kufuatia kupanda kwa bei za mafuta hapo awali licha ya kupunguza kutoka katika bei ya awali ya 3,600 hadi kufikia 3400 kwa sasa,"amesema.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kupunguza bei ya mafuta waweze kujipatia kipato kama ilivyokuwa huko nyuma ili kuendelea kuimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja lengo ni kuwawezesha wananchi kumudu gharama za maisha,amesema Juma.
Aidha, aliwaomba makondakta wa mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kujiunga kwenye chama hicho ili waweze kupata fursa zinazotolewa ikiwemo kupata elimu zitakazo wawezesha kufanya kazi kwa weledi,uaminifu,kufuata sheria na taratibu na kusaidia kwenye shida na raha.