Polisi wakutana na makubwa Pwani, waliohujumu TANESCO wadakwa

NA ROTARY HAULE

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 57 kwa makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo kuharibu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na kusababisha hasara zaidi ya milioni 76.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Gregory Mushi amewaambia waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa, watuhumiwa hao wamekamatwa katika wakati tofauti wakati Jeshi likiwa katika operesheni maalum ya kusaka wahalifu.

Mushi amesema kuwa, Julai 3, mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi maeneo ya Vikuruti Kitale Kata ya Mlandizi Tarafa ya Mlandizi Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (TANESCO) lilimkamata mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 39 mkazi wa Mlandizi akiharibu miundombinu ya shirika hilo.
Mushi amesema, alikamatwa akiwa anaharibu miundombinu hiyo kwa kukata line ya umeme ya msongo wa 33KV ambao ulikuwa unamhudumia mteja anayejulikana kwa jina la Swai.

Mushi ameongeza kuwa, mtuhumiwa huyo alitumia mbinu ya kuchoma moto nguzo na kupelekea line hiyo kuanguka na kuiba waya wa alminium ACCR 100 MM na kulisababishia Shirika hasara ya zaidi ya milioni 76.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeendesha oparesheni katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa na kufanikiwa kuwakamata wahutumiwa 57 ambao wamejihusisha katika matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme,usafirishaji dawa za kulevya,ubakaji,na vitendo vya ukatili,"amesema Mushi.

Ofisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Pwani, Mohamed Kitoro amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wa kumkamata mtuhumiwa huyo huku akiomba waendelee kushirikiana katika kudhibiti vitendo vingine vya kihalifu dhidi ya miundombinu hiyo.

Kitoro ametoa wito kwa wananchi kuacha kuharibu miundombinu ya Serikali na kwamba watoe ushirikiano pale wanapoona watu wakiharibu miundombinu hiyo.

Aidha,katika matukio mengine Jeshi hilo limekamata mtu mmoja mwanaume (48) Mkazi wa Makambako mkoani Iringa akisafirisha mirungi bunda 150 zenye uzito wa Kilo 70 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro kuelekea Tunduma Mkoa wa Songwe kwa kutumia gari lenye namba za usajili T.254 DDY aina ya Toyota IPSUM.
Hata hivyo, watuhumiwa wengine wamekamatwa kwa kosa la ubakaji na kusababisha kifo cha mtoto pamoja na vitendo vya ukatili vinavyomhusisha mfanyakazi wa ndani kummwagia mafuta ya moto na kumjeruhi katika sehemu za usoni na mkono wa kulia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news