NA MATHIAS CANAL
MBUNGE wa Jimbo la Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda leo Julai 19, 2022 ameanza ziara ya kikazi ya siku saba jimboni kwake Rombo mkoani Kilimanjaro.

Amesema kuwa, kipindi cha nyuma kulikuwa na kampuni ya Kili Water ilioanzishwa kama kampuni ya kutoa huduma ya maji Rombo, lakini haikuwa na uwezo wa kutoa maji ya kutosha.

Prof.Mkenda amesema kuwa katika hatua za kuimarisha upatikanaji wa maji serikali iliamua kuanzisha Bodi ya Maji Rombo inayoitwa ROMBOWASA ambayo inawajibika kutengewa bajeti na serikali kwa ajili ya sekta ya maji.
Mbunge huyo amesema kuwa kufuatia kuanzishwa kwa ROMBOWASA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 10 kwa wananchi wa Rombo kwa ajili ya upatikanaji wa maji ambapo hadi sasa wataalamu wanaangalia vyanzo vya maji ili kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi.

"Rais Samia ameamua na amekusudia kuhakikisha maji yanapatikana na ndugu zangu wananchi nawahakikishia kuwa tuna Rais imara, mchapa kazi na hata waangusha wanachi wake kamwe,"amesema.
Prof.Mkenda amesema kuwa, katika ziara hiyo amekusudia kuwaeleza wananchi umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Waziri wa Maji, Mhe.Juma Aweso za kumtua ndoo mama kichwani.