NA OR-TAMISEMI
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe ametembelea Shule ya Wavulana ya Tabora na Shule ya Wasichana Tabora kukagua viwanja vya michezo vitakavyotumika katika Mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA kwa mwaka 2022.
Katika ukaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, Prof. Shemdoe ameelekeza Kamati ya Maandalizi ya Michezo hiyo kuhakikisha masuala muhimu yote yanakamilika kabla ya kuanza mashindano hayo kuanza.
‘Nahitaji kuona maandalizi ya viwanja vyote vitakavyotumika katika mashindano hayo pamoja shule zitakazotumika kwa ajili malazi kukamilika mapema kusubiria siku ha ufunguzi wa mashindano hayo,’ amesisitiza Shemdoe.
Idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kushirikia mashindano hayo kwa mwaka huu wa 2022 ni 3600 kwa upande wa UMISETA na 3320 kwa upande wa UMITASHUMTA Tanzania Bara na Visiwani.
"Hakikisheni maandalizi ya viwanja na malazi yote yanakamilika haraka ili watoto watakapofika wafurahie kushirikiki katika mashindano hayo makubwa yanayolenga kukuza vipaji vya watoto kimichezo,"amesema.
Katika hatua nyingine baadhi ya walimu wa shule za Mkoa wa Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi na mazingira ya kujifunza na kufundishia.
Mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika kuanzia Julai 29 hadi Agosti 9, 2022 na UMISSETA yatanguruma kuanzia tarehe 9 hadi 19 mwezi Agosti,2022.