NA DIRAMAKINI
MKURUNGEZI wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Mhandisi Charles Sangweni amesema Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) katika Mkoa wa Lindi unatarajia kuanza mwaka 2025 huku gesi ya kwanza kuanza kuuzwa 2030 iwapo hakutakuwa na vikwazo vya uzalishaji.
Pia amesema, mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 70 ni mkubwa utawavutia wawekezaji wengi zaidi wa utafutaji wa mafuta na gesi hapa nchini.
Mhandisi Sangweni ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.
"Mradi huu umekuja baada ya Serikali kufanya maamuzi ya makusudi kwamba gesi ambayo imegundulika kwa wingi kwenye kina kirefu cha bahari ibadilishwe kutoka katika hali ya hewa na kuwa kimiminika ili iweze kubebwa kwenye mitungi na kwenda kuuzwa Mashariki ya Mbali kama Japani, China na nyinginezo ambazo zimeonekana kuhitaji,"amesema.
Pia amesema katika kuhakikisha mradi huo unaanza Juni 11, mwaka huu waliingia makubaliano ya awali ya utekelezaji wa muundo wake pamoja na sheria iweje na kwamba majadiliano hayo yakikamilika wanatarajia Desemba, mwaka huu watasaini mkataba uliokamilika.
Vilevile amesema,baada ya mkataba rasmi kukamilika wanatarajia kwenda kwenye kazi nyingine kama usanifu wa mradi na namna ya kupata fedha za utekelezaji.
“Kama mradi huu utazalisha gesi kwa miaka 30 na kipindi cha ujenzi utaleta ajira zaidi ya watu 10,000 huku ajira za kudumu zitakuwa zaidi 600,”amesema.
Pia amesema kupitia mradi huo wa LNG viwanda vingi vitajengwa kwa sababu ujenzi wa mradi huo utahitaji vifaa vingi vikiwemo nondo, simenti na vitu vingine mbalimbali, "kwa hiyo sisi kama PURA tumeona ni wakati sahihi sasa wa kusimamia kauli mbiu ya Tanzania ni mahali sahihi pa uwekezaji,” amesema.
Aidha amesema wakati PURA inaanza mwaka 2015, kampuni za kigeni zilikuwa zinaajiri watanzania chini ya asilimia 50 ila kwa sasa walioajiriwa kwa nafasi zotè wameongezeka na kufikia asilimia 90.
“Lakini hata kwenye manunuzi, sasa hivi bidhaa nyingi zinazonunuliwa, ushirikishwaji wa kampuni za kitanzania kwenye sekta hii ya mafuta na gesi umekuwa kwa kiasi kubwa na hiyoinatokana na juhudi za watanzania wenyewe ambao wamekuwa wajielimisha pamoja na vyuo vyetu kutoa elimu juu ya mafuta na gesi,”amesema.
Amesisitiza kuwa, wao kama PURA wapo katika maonesho hayo kwa lengo la kuwaeleza wananchi fursa zinazopatikana katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi hapa nchini pamoja na kutoa elimu juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo.
“PURA kwa kuanzia tunawaeleza juu ya uhushishaji wa watanzania kwenye shuguli hizi za utafutaji wa mafuta na gesi, tunaona sasa ni wakati sahihi wa kueleza jamii kwanini Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji,”amesema.