NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufanya uchunguzi ili kubaini namna Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Associated Investment Company Limited alivyopata kazi ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari Mtopepo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akifuatana na Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe.Masoud Ali Mohamed (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa wakati alipowasili katika viwanja vya Karakana katika uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa mabanda ya Biashara za Wajasiriamali yaliyojengwa kupitia mkopo wa UVIKO 19,akiwa katika ziara ya Wilaya ya Mjini,Mkoa wa Mjini Magharibi leo.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo wakati alipozungumza na viongozi, watendaji wakuu na maofisa wa serikali baada ya kukamilisha ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendeshwa kupitia Fedha za Ahueni za Uviko -19 pamoja na miradi mingineyo.
Amesema, katika mradi huo Mkandarasi huyo amebainika hana uwezo, hivyo kuna umuhimu wa ZAECA kufanya uchunguzi ili kubaini namna alivyopata kazi hiyo, kwani kuna mashaka kuwa huenda alipata kazi hiyo baada ya kuweka kiwango cha chini cha gharama za ujenzi au mbali na kujulikana kuwa hana uwezo; alipewa kazi hiyo baada ya kutoa rushwa.
Alisema, mbali na kubainika changamoto hizo katika ziara hiyo, pia kumebainika kuwepo changamoto katika ujenzi wa masoko, hivyo akaitaka sekta binafsi kuwa na uhakika wa uwezo wa wakandarasi kabla ya hatua ya kukabidhi miradi.
Amesema, Serikali imefanya uamuzi wa kuendeleza mradi wa ujenzi wa Masoko ya Jumbi, Mwanakwerekwe pamoja na Chuini kwa kikosi cha JKU baada ya kugundua kuwa Sekta binafsi ilishindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Hata hivyo, alikitaka kikosi hicho cha JKU kufanya kazi ya kujenga masoko hayo kwa spidi kubwa; usiku na mchana kwa kuzingatia Serikali iliwaweka pembeni wafanyabiashara ili kupisha ujenzi huo.
Aidha, amezitaka Idara za Manispaa kuweka fedha za kutosha katika kuendeleza miradi ya maendeleo kutokana na makusanyo wanayofanya, kwa kigezo kuwa fedha zinazotengwa hivi sasa hazikidhi mahitaji ya kuendesha miradi.
Amesitiza umuhimu wa manispaa kupambana na changamoto ya uchafu katika maeneo mbalimbali ya barabara na maeneo ya Mji, hususan maeneo ya ndani, huku akisisitiza azma ya serikali ya kuzibadili taka kuwa rasilimali zenye thamani.
Mapema Rais Dkt. Mwinyi alitoa tathmini ya maendeleo ya miradi aliyoitembeela kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo ya afya.
Amesema, kuna maendeleo mazuri yaliofikiwa katika uendelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Hospitali za Wilaya pamoja na ile ya mkoa iliyopo Lumumba na kubainisha matumaini yake ya kukamilika ujnezi huo na kuzinduliwa katika kipindi cha Sherehe za Mapinduzi, Januari 12, 2023.
Aliutaka Uongozi wa Wizara ya Afya kuhakikisha vifaa vyote vinavyojhitajika katika Hospitali hizo vinapatikana kwa wakati.
Aidha, aliutaka uongozi huo kuhakikisha unafanikisha Ajira aa Wafanyakazi wa Hospitali hizo kwa kuzingatia kuwa tayari Serikali imeshaidhinisha suala hilo, ikilenga kuhakikisha kunawepo utoaji wa huduma bora zaidi za Afya, hususan katika kupunguza Vifo vya mama na watoto.
Aliiagiza Wizara hiyo kuandaa bajeti ili kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora katika maeneo ya hospitali pamoja na kujenga uzio, sambamba na kuweka utaratibu wa kuwaondoa watu wanaofanya shughuli mbalimbali karibu na maeneo ya hospitali.
Vile vile alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinaboreka katika nyanja zote kwa kuzipatia vifaa, miundombinu, wafanyakazi, dawa pamoja na vifaa tiba, huku akiitaka Wizara Afya kuboresha Bohari ya Madawa ili kuwa na matandao wa kisasa wa Huduma za Afya (ICT) ili mashine mbali mbali ziliopo kama vile MRI ziweze kusomwa popote pale.
Akigusia sekta ya Elimu, Dkt. Mwinyi alisema mbali na kasoro zilizobainika katika Skuli ya Sekondari Mtopepo, kwa ujumla maendeleo ya miradi katika sekta hiyo ni ya kuridhisha.
Alisema anafuraha kuona Serikali inajenga Skuli za kisasa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, zikiwa na maabara, maktaba pamoja na vyumba vya kompyuta.
Alitumia fursa hiyo kulipongeza Jeshi la kujenga Uchumi (JKU) kwa kufanya vizuri katika ujenzi wa skuli mbali mbali, na kwa gharama nafuu na hivyo akaitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kujipanga katika suala la upatikanaji wa vifaa pamoja na kufanikisha Ajira za walimu na kusema skuli hizo nzuri zinahitaji kuwa na uzio pamoja na kuwepo katika mazingira bora.
Aidha, aliagiza Wizara hiyo kuhakikisha viwanja vyote vya michezo vilivyotumika kwa shughuli za miradi kunakuwa na mbadala wake na kusema ni lazima kufanyike ujenzi wa viwanja vya kisasa vya michezo.
Kuhusiana na Sekta ya Maji, Dkt. Mwinyi alisema haridhishwi na upatikanaji wa huduma ya maji na kutaka juhudi zifanyike kuhakikisha maeneo yote yasiokuwa na huduma hiyo zinapata maji.
AliitakaWizara ya Maji, Nishati na Madini pamoja na ZAWA kujipanga na kuhakikisha maeneo yote ya mkoa yanapata maji baada ya Mradi wa Exim Bank ya India utakapokamilika.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwinyi amesema, kumekuwepo maeneo finyu kwa shughuli za wafanyabaishara kiasi cha kuzorotesha shughuli hizo, hivyo akazitaka Idara za Manispaa kutafuta fedha ili kupanua wigo wa maeneo ya kufanyia biashara hizo.
Alisistiza umuhimu wa manispaa kuwa na ubunifu katika kupata mikopo itakayowezesha kuwa na miundo mbinu ya kutosha ya kufanyia biashara, huku akiahidi Serikali kuwa tayari kuweka dhamana.
Kuhusiana na Uchumi wa Buluu, Dkt. Mwinyi alisema lengo la Serikali ni kuwapatia wavuvi mambo kadhaa, ikiwemo zana za kuvulia, masoko, vyumba vya baridi, bandari za Uvuvi sambamba na kuwepo Vyumba vya kuchakata samaki.
Alizitaka taasisi zinazohusika kuwa na ubunifu na kutafuta wawekezaji pamoja na kupata mikopo ili kuwawezesha wananchi katika sekta hiyo na kusema wananchi walio wengi hapa nchini ni wavuvi.
Akizungumzaia sekta ya ujasiriamali,Rais Dkt. Mwinyi alisema serikali itaendelea kutoa mikopo na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hizo kwa kigezo kuwa kuna fedha za kutosha zilizotengwa kwa ajili hiyo.
Aidha, altumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kusimamia uwepo wa miradi mbali mbali ya Uwekezaji kupitia sekta binafsi kiwemo ujenzi wa skuli za kisasa nyumba za kukodisha pamoja na maduka.
Sambamba na hayo, Dkt. Mwinyi aliupongeza kwa dhati uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi kwa kusimamia vyema majukumu yao pamoja na viongozi (mawaziri) kutoka Kambi ya Upinzani kwa kigezo cha kufanya kazi kwa juhudi kubwa.
Nae, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa pamoja na kutoa shukrani kwa viongozi, watendaji na wananchi wa mkoa huo kwa kushiriki kikamlilifu katika ziara hiyo, alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara na wananchi kutoa na kudai risiti wakati wanapofanya manunuzi.