Rais Dkt.Mwinyi akamilisha ziara yake mikoa yote, atoa maagizo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekamilisha ziara yake katika wilaya zote za Unguja na Pemba na kueleza jinsi alivyoridhika na hatua iliyofikiwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoitembelea.
Rais Dkt.Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akitoa majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kusini Pemba, ambapo leo anakamilisha ziara yake ya Mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba iliyoanza Julai 16, 2022 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Makonyo, Wawi Chake Chake katika Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema kwamba, madhumuni ya ziara hiyo ni kupita katika Mikoa na Wilaya zikiwemo wilaya ndogo na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya UVIKO-19 pamoja na kufanya tathmini ya Ilani ya Uvhaguzi ya CCM na kusema kwamba lengo lake la kufanya ziara hiyo limetimia kwa mafanikio makubwa.“Namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kukamilisha ziara yangu katika mikoa yote”.

Amesema kwamba, miradi mbalimbali aliyoitembelea na mengine kuiwekea mawe ya msingi ameridhika nayo katika uendelezaji wake isipokuwa mradi mmoja tu ambao haukufikia lengo lililokusudiwa.

Alitoa pongezi kwa mkoa huo kwa kuendeleza amani na usalama katika mkoa huo na kuwaeleza kwamba wananchi wanapaswa kupewa pongezi kubwa kwani hivi sasa wameungana na kuwa wamoja.Amesema kuwa, maendeleo yote yanayozungumzwa hayawezi kupatikana kama hakuna umoja, amani na usalama.

Rais Dkt. Mwinyi alimpongeza Mkuu wa Mkoa na kusema kwamba yale maono yake ifike pahali wakuu wa mikoa kuonesha mipango na alichofanya ndicho kinachotakiwa na kuahidi kwamba Serikali itamsaidia.

Alieleza kwamba kama alivyoeleza katika mikoa mengine, bado anataka hatua zaidi ziimarike katika mabaraza ya miji na atakapokuja tena mara ya pili anataka kuja kuzindua miradi ya mabaraza ya miji.

Ameyataka mabaraza ya miji kuwa na utaratibu mzuri wa kukusaya mapato na kuwataka kuwa na maono na kueleza namna Serikali itakavyoweka msaada katika kuwasaidia kwenye mikopo.

Alisema kwamba, ujenzi wa “Mkoani Complex” ni kitu kizuri kilichobuniwa na mkoa huo na kuwataka angalau asilimia 30 iende kwenye maendeleo kwani tayari suala la madiwani limeshachukuliwa na serikali kuu.

Alisema kwamba, miradi yote aliyoitembelea imefikia hatua nzuri na kuwapongeza wote waliosimamia miradi hiyo wakiwemo wafanyakazi katika ngazi za wilaya, mkoa, pamoja na wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kwamba Wilaya ya Mkoani pekee ndio hawajapata hospitali ya wilaya na hiyo ni kwa sababu Serikali imeamua kwa makusudi kuiboresha Hospitali ya Abdalla Mzee.

Alieleza hatua zinazoendelea katika kuimboresha hospitali hiyo ambapo leo aliizindua sehemu ya kusafisha damu za wagonjwa wa figo yenye vitanda vitano ambayo ni ya kisasa na tayari ameanzisha safari ya kuimarisha hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka Xray ya kisasa pamoja na gari inayotumia umeme kwa ajili ya wagonjwa .

Alisema kwamba, Hospitali ya Abdalla Mzee itawekewa vifaa na kuwataka wizara ya afya kuendelea kutoa vifaa pamoja na watoa huduma za afya.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais Dkt. Mwinyi aliitaka Wizara ya Elimu kutekeleza mpango mwingine wa kazi waliyoianza katika kuimarisha sekta hiyo kwani bado kuna mahitaji.

Kwa upande wa sekta ya maji alisema kuwa, asilimia ya maji yanayopatikana hivi sasa ni 50 tu Unguja na Pemba hivyo, ni lazima kazi ya ziada ikafanywa na kueleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali zikiwemo njia mbadala na kueleza kwamba tatizo la maji litaondolewa Unguja na Pemba.

Rais Dkt. Mwinyi alimtaka Waziri wa Fedha kuhakikisha anamaliza suala zima la fidia kwani wananchi walio wengi ni masikini ili kazi zifanyike na wananchi wasinungunike.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya CRDB kwa kufanya kazi nzuri ya dhamana waliyopewa na Serikali katika kutoa mikopo kwa wajasiriamali.
Aliwashukuru wananchi waliokubali kutoa vipando vyao kwa ajili ya kujenga barabara na kuwashukuru kwa uzalendo wao na kueleza jinsi atakavyotafuta fedha za ziada ili zipate kuongezwa na barabara nyingine.

Akieleza kuhusu uchumi wa buluu, Rais Dkt. Mwinyi alisema kwamba, bado hajaridhika na ufugaji wa samaki, kaa na majongoo unaofanywa na kuitaka Wizara husika kuwasaidia wafugaji hao ikiwa ni pamoja na kuwatafutia vifaranga.

Alisisitiza haja ya kuongeza mikarafuu na kuitaka ZSTC kuja na mpango maalum wa kuongeza zao hilo ikiwa ni pamoja na kupanda mikarafuu mipya na kuongeza pembejeo katika zao hilo.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza miongoni mwa miradi mikubwa inayokusudiwa kuimarishwa na Serikali anayoiongoza huko kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ambao utasaidia kuifungua Pemba ambapo ndege zote kubwa zitaweza kutua kisiwani humo.

Alizieleza hatua nyengine zitakazochukuliwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Pemba na kueleza hamu yake ya kuona mradi mkubwa wa bandari unaimarishwa badala ya uliopo hii sasa na kuona meli zinazotoka Dubai na sehemu nyenginezo zinafunga gati katika bandari hiyo.

Alieleza hatua ambazo zinazochukuliwa katika ujenzi wa barabara kuu zikiwemo barabara ya Cheke- Mkoani na Chake- Wete pamoja na kuweka eneo maalum la viwanda katika eneo la Chamanangwe kisiwani Pemba.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kwamba baada ya ziara hiyo kilichobaki ni kazi na kuhakikisha miradi yote aliyoahidiwa inamaliza kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news