Rais Dkt.Mwinyi akoleza kasi ya uchumi wa buluu Pemba, akabidhi vitendea kazi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekabidhi boti 57 na mashine 32 kwa wavuvi na wakulima wa mwani zenye thamani ya shilingi milioni 783 kwa wanufaika 914 wa Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi boti ya uvuvi kiongozi,Faki Mpemba Faki kwa ajili ya uvuvi wa samaki, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Soko la Samaki Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba.(Picha na Ikulu).

Boti hizo 42 za wakulima wa mwani Wilaya ya Micheweni na vifaa vyake, 15 za wavuvi na hundi ya shilingi milioni 210 kwa Kikundi cha Shirikani Cooperative Society imetolewa na Benki ya CRDB kupitia mikopo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo imedhaminiwa na Serikali kupitia fedha za UVIKO-19.

Akizungumza na wananchi wa Tumbe katika hafla ya kukabidhi boti hizo Dkt.Mheshimiwa Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar ni nchi ambayo imezungukwa na bahari na Serikali iliposema uchumi wa buluu imekusudia kuitumia vyema Bahari kwa kilimo cha mwani, uvuvi na mengineyo.

Ameeleza kuwa, Serikali imepanga kutoa boti za uvuvi 577 kwa Zanzibar ambapo boti nyingi zinatarajiwa kutolewa kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba, lengo lake ikiwa ni kuwawezesha wakulima wa mwani na wavuvi kupata zana za kisasa, kupata elimu, mitaji na maeneo mazuri ya kufanya biashara zao.

"Tumetoa boti za ukulima wa mwani zenye mashine zake 500 kwa Zanzibar kuwasaidia wakulima wa wasipate shida ya kubeba mwani wao, leo tunakabidhi boti hizi za mwani, uvuvi na mashine 32 kwa wananchi,"amesema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na mkewe Mama Mariam, wakitembelea chumba cha kugandisha barafu katika Soko la Samaki Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba baada la kulifungua rasmi Soko hilo Julai 26,2022 akiwa katika ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, kutembelea miradi ya maendeleo.

Ameeleza, ahadi alizozieka kwa wananchi sasa zimeanza kutekelezwa kwa kuwapatia wajasiriamali mitaji, vifaa, na kuwajengea masoko yenye mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

"Tuliposema tutatoa ajira laki 300,000 katika miaka mitano hii ilikuwa ni ajira zinazotokana na kuwawezesha wananchi leo tumewawezesha wakulima wa mwani na wavuvi lengo letu wananchi wajiajiri wenyewe,”amesema.

Amesema, boti hizo zitakuwa na majokofu yenye uwezo wa kuhifadhi samaki tani moja kwa siku, ili kuwawezesha wavuvi kurudi na samaki wao bila ya kujali kuharibika.

"Baada ya kukamilika kwa kiwanda cha mwani pale Chamanangwe wakulima wa mwani mtapata bei ya uhakika na sio ile bei ya kutupa ya zamani tuendelee kuhamasishana ili wananchi waondokane na njaa na umasikini,"amesema.
Aidha, aliwahakikishia wavuvi kwamba Serikali ina uwezo wa kutoa boti kubwa zenye uwezo wa kuhifadhi samaki tani tano na 10 yenye uwezo wa kubeba wavuvi 60 alisema, huu ni mwanzo serikali yao inauwezo wa kufanya hivyo endapo watakua waaminifu.

Akitoa taarifa fupi ya Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Waziri wa wizara hiyo Zanzibar Mudrik Ramadhan Soraga alisema, kazi hiyo imeratibiwa na wizara yao wakishirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kulifungua Soko la Samaki Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba na kushoto kwa Rais ni mkewe Mariam Mwinyi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said.

"Matumaini yangu kutokana na harakati hizi wananchi ni dhahiri wanaendelea kufaidi matunda ya Serikali yao ambayo lengo lake ni kuwawezesha katika harakati mbalimbali za kimaendeleo,"amesema.

Akiwa Tumbe ambako Rais Dkt.Mwinyi alilizindua soko la Tumbe na kukabidhi boti, mashine za boti, kwa wavuvi, vifaa vya kupandia mwani, pamoja na kukabidhi hundi ya shilingi milioni 210.8 kwa kikundi cha Shirikani Cooperative Society alieleza lengo la serikali la kuwawezesha wajasiriamali ili waweze kujiajiri wenyewe na kufikia idadi ya azma ya ajira laki tatu zilizoahidiwa.

Alisema kuwa, Serikali imeamua kwa makusudi kuwawekea wavuvi mazingira mazuri ili waweze kupata tija katika katika shughuli zao.

Nae Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud Makame alisema, ujenzi wa mabwawa ya samaki, kaa, majongoo bahari, wavuvi na wakulima wa mwani Mkoa wa Kaskazini Pemba umechukua asilimia 45.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wananchi wa Tumbe wakati wa hafla ya kukabidhi boti kwa wavuvi wa samaki na wakulima wa mwani wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati wa ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kutembelea miradi ya maendeleo.

"Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba tuna jumla ya boti 337 za mwani ambapo kwa Zanzibar boti zote ni 500 hivo tumeona Mkoa huu ulivoweza kunufaika katika kuimarisha zao la mwani na vifaa hivi vitakwenda kuondoa changamoto kubwa ambayo imekua zikiwakabili wakulima hawa," alisema.

Akitoa tathmini ya kazi hiyo Mwakilishi wa Banki ya CRDB Zanzibar alisema, vifaa hivyo ni boti 42 za mwani, boti 15 za uvuvi ambapo jumla ni 57 zenye thamani ya TZS milioni 783 zitatolewa kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni.

"Tuna boti 94 ambazo zimefanikiwa kutolewa sehemu mbali mbali ikiwemo Tumbe na kati ya boti hizo 57 ndio hizi na 36 zitapatikana Mkoa wa Kusini Pemba kadri ziara ya Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwinyi inavoendelea," alisema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa wananchi hao wanatakiwa kuthamini misaada hiyo kwa kuitumia ipasavyo ili iwe endelevu kwa ajili ya kukuza vipato vyao.

Mapema Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi katika skuli ya Sekondari Makangale na kumpongeza mkandarasi wa ujenzi wa skuli hiyo kwa kazi nzuri huku akimtaka akamilishe kazi hiyo kwa kipindi kifupi ili wanafunzi wapate kuendelea na masomo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 210.8 Mwenyekiti wa Kikundi cha Uvuvi cha Kiuyu Mbuyuni Pemba, Hatibu Khamis Faki ikiwa ni mkopo uliotolewa na Benki ya CRDB kwa kikundi hicho, hafla hiyo ilifanyika katika viwanja Soko la Samaki Tumbe.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohammed Mussa, kwa upande wake alisema kuwa Serikali imekua ikijenga skuli za nyingi kwa ajili ya kupunguza msongomano wa wanafunzi.

"Skuli hii ya Ghorofa mbili yenye madarasa 21 itapunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi kwenye madarasa wanafunzi watakaa 40 kwenge chumba kimoja ili wawe wanasoma katika mazingira mazuri," alisema.

Rais Dk. Mwinyi akiwa Tumbe mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa Wajasiriamali wa ujenzi wa Majengo ya Wajasiriamali, alikipongeza kikosi cha KMKM kwa kufanya kazi vizuri na kuahidi kuendelea kuwapa kazi zilizobaki katika mradi huo.

Pia, aliahidi kupatiwa umeme wananchi waliocheleweshewa huduma hiyo, ujenzi wa barabara yao ya Finya huku akieleza kwamba hatua zitachukuliwa katika kuhakikisha wananfunzi wa skuli za msingi wanaofanya vizuri nao wanapewa zawadi

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alifika Kilindi katika mradi wa ujenzi wa Tangi la kuhifadhi maji ambapo litakuwa na ujazo wa lita milioni moja na kuwaahidi wananchi kupata maji safi na salama na kuwatakuwa kwua na subira.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zilizowasilishwa na viongozi wao.

Nae Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za maendeleo anazozichukua kwa ajili ya wananchi ambazo na wao wakiwa ni sehemu ya chama hicho wanaziunga mkono huku akipongeza mashirikiano yaliyokuwepo kati ya Serikali na chama katika Mkoa huo.

Alieleza matumani ya chama hicho katika mkoa huo kwamba hadi ifikapo mwaka 2025 Rais Dkt.Mwinyi atakuwa tayari ameshamaliza utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na nyongeza atakayoifanya ya utekelezaji kwa kiasi kikubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news