Rais Dkt.Mwinyi aongoza Mahafali ya 10 Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), asisitiza jambo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kuwepo kwa changamoto za kiusalama katika Taifa moja kunaweza kuleta athari kwa maendeleo na ustawi wa mataifa mengine.
Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika Mahafali ya 10 ya Wahitimu wa mwaka 2021/2022 wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kinachotoa mafunzo ya Usalama na Stratejia,hafla iliyofanyika Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, mfano mzuri ni hivi sasa ambapo kuna mgogoro baina ya mataifa ya Urusi na Ukrane.

Ameongeza kuwa, vita hii imeathiri sana uchumi wa dunia kwa kusababisha pamoja na mambo mengine changamoto ya ongezeko la bei za bidhaa, usalama wa chakula, uhamiaji, uhusiano wa Kimataifa pamoja na kutetereka kwa hali ya kisiasa nje ya mataifa hayo.

Ameeleza kuwa, katika kukabiliana vizuri na changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa, itategemea sana namna Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilivyojitayarisha kukabiliana na hali hiyo pamoja na uhusiano na mataifa mengine.

Kwa msingi huo, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, chuo hicho kinachofundisha masuala muhimu ya kiulinzi na kiusalama kina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, kuwepo na kuendelea kudumu kwa hali ya amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lole.

Ameongeza kuwa, ni dhahiri kwamba chuo hicho kinachofundisha mafunzo juu ya masuala muhimu ya kiulinzi na kiusalama kina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kuwa, chuo hicho ni muhimu hasa kwa wakati huu ambapo Dunia imekabiliwa na changamoto na matishio mengi ya kiulinzi na kiusalama ambapo miongoni mwa matishio hayo ni vitendo vya kigaidi, vita na migogoro baina ya mataifa, vita vya wenyewe kwa wenyewe, wizi wa kimtandao, biashara na matumizi ya dawa za kulevya, uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mafanikio ya kitaaluma ya chuo chochote kile yanategemea sana juhudi za chuo katika kufanya tafiti mbali mbali na kuweka mkazo wa matumizi ya tafiti hizo kwa maendeleo ya chuo na jamii kwa jumla.

Amesema kuwa, kuna masuala muhimu ya ulinzi na usalama yanayohitaji kufanyiwa utafiti wa kina ili kuweza kukabiliana nayo hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuweka mkazo katika kufanya tafiti mbali mbali pamoja na kutumia na kusambaza matokeo ya tafiti hizo kwa maendeleo na maslahi ya Taifa.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, ndani ya kipindi cha miaka 10 chuo hicho kimeendesha programu mbalimbali kwa viongozi wa ngazi za juu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wa taasisi nyingine za Serikali.

Amesema kuwa, Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinapongeza na kufurahia kuona kwamba hivi sasa wapo maafisa wengi ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za Serikali ambao wamepata mafunzo kutoka chuoni hapo na baadae kukabidhiwa nafasi nyeti na muhimu za uongozi.

Katika hotuba yake, Rais Dkt.Mwinyi ameongeza kuwa, wamekabidhiwa nafasi hizo wakiaminika kwamba wamepikwa vyema na ndiyo maana wote wamekuwa wakifanya vizuri katika nafasi wanazokabidhiwa. 

Amewatakia mafanikio washiriki wa mafunzo maalumu ya 13 yatakayoendeshwa mwaka huu ambayo yatajumuisha Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za Serikali.
“Nina imani kwamba washiriki wote hao watafurahia fursa walioipata ya kushiriki mafunzo hayo ambayo yametayarishwa ili yakidhi mahitaji ya kazi zao na muda walionao, nawahimiza washiriki wote waitumie vizuri nafasi hiyo,”amesema Dkt. Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, hakuna Taifa lenye kujitosheleza lenyewe peke yake, kwa msingi huo alitoa pongezi kwa uongozi wa chuo hicho kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mataifa mengine katika ngazi ya kikanda na Kimataifa.

Pia amesema kuwa, ni habari njema kujua kwamba chuo hicho kinaendelea kuvutia washiriki wa mafunzo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya SADC, nchi za Nigeria, Misri na nchi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika.

Amesema kuwa, uhusiano ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, kiulinzi na kiusalama na ni dhahiri kwamba maendeleo ya Taifa lolote lile yanategemea sana ushirikiano na uhusiano wake na mataifa mengine wka hivyo, aliunasihi uongozi wa chuo hicho kuendeleza juhudi hizo za kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo.

Alitoa shukurani kwa uongozi na Jumuiya ya Chuo kwa kuendelea kufanya ziara za masomo za kwenda Zanzibar kila mwaka ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya chuo hicho.

Amesema kwamba, ziara hizo hutoa fursa ya kujifunza historia pamoja na kuona vivutio kadaa vya utalii vilivyopo Zanzibar.

Sambamba na kusikiliza uwasilishwaji wa mada zinazohusu masuala mbali mbali ya kisera, kiuchumi na kisiasa na kujionea hatua za utekelezaji wa mipango ya maendeleo ukiwemo uchumi wa buluu.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ulinzi na Usalama cha Taifa (NDC), Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona ameeleza mafanikio yaliopatikana katika chuo hicho ambapo kwa mwaka huu wahitimu wake ni 43.

Alieleza hatua watakazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha wanaendeleza ushirikiano na Serikali zote mbili ile ya Jamhuriya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuwa, mafunzo hayo ni ya wiki 47 ambapo chuo hicho hutoa elimu ya masuala muhimu ya kimkakati katika nyanja ya ulinzi na usalama kwa viongozi mbalimbali.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alitoa vyeti na zawadi kwa wahitimu ambapo kwa upande wa zawadi waliopata zawadi ni Naomi Zegezege Mpenda kutoka Tanzania aliyepata ushindi wa kwanza, Richard Connie Wakayinja kutoka Uganda, Bernard Mutasa kutoka Zimbwabwe, Chehu Muhammad Chindo kutoka Nigeria na wa tano ni Haycall Clive Mughanga kutoka Kenya.

Mapema Rais Dkt.Mwinyi alitoa vyeti na Beji ya Tuzo ya Fahari kwa wahitimu wote wa mwaka 2021/2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news