NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inaendelea kuziondoa changamoto zote kwenye sekta ya elimu ili watoto wote wa Zanzibar waweze kupata elimu katika mazingira bora.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti mara baada ya kuweka mawe ya msingi katika skuli ya ghorofa ya msingi Mwambe sambamba na ufunguzi wa skuli ya Ng'ombeni “A”, Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.
Ameeleza kuwa, kutokana na uhaba wa madarasa ya kusomea kwa wanafunzi katika maeneo mbalimbali Serikali imeamua kujenga majengo mbalimbali yakiwemo ya ghorofa ili kuondoa tatizo hilo.
Alifahamisha kuwa, elimu ndio msingi wa kuleta maendeleo nchini na hakuna taifa lolote lililoendelea duniani bila elimu hivyo, ni vyema kuendelea kuitilia mkazo sekta hiyo.
"Tutaendelea kuijenga majengo ya skuli ya ghorofa, kuijenga majengo ya kawaida, kukarabati majengo yaliyochakaa pamoja na kumalizia yale ambayo yalishaanzwa kujengwa,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Akizungumzia matatizo ya maji na barabara huko Kendwa jimbo la Kiwani, Dkt. Mwinyi amesema, Serikali itafanya kila inalowezekana kuhakikisha matatizo yote ndani ya jamii yanaondoka na wananchi kuishi maisha bora.
Amesema kitu muhimu katika maisha ya binadamu ni maji na kuahidi kuwa Serikali inaunganisha mpango mpya wa kuijenga barabara za ndani ili kuwaondolea usumbufu wananchi.
Akizungumza na wajasiriamali huko katika bandari ya Mkoani, Rais Dkt. Mwimyi amesema Serikali itahakikisha inawawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia elimu hiyo, mitaji na masoko ili waweze kuendeleza na shughuli zao bila matatizo.
Wakati huo huo, Dkt. Mwinyi aliwasisitiza wananchi juu ya kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo Agosti 23 kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Leila Mohamed Mussa alisema uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga majengo ya skuli ya gorofa ni moja kati ya mkakati wa kuimarisha huduma za elimu.
Alifahamisha kuwa, ili wanafunzi waweze kupata elimu bora hakuna budi kuishukuru Serikali kwa juhudi zake hizo.
“Wananchi lazima tumuunge mkono Rais wetu kwa mema anayoendelea kutuletea katika maeneo yetu mbalimbali yanayoendana na maendeleo ya kijamii,”alieleza.
Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud Makame alisema zoezi la kuwawezesha wajasiriamali, wavuvi na wakulima wa mwani litawapatia tija na kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Katika ziara yake hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuzinduwa kliniki ya usafishaji na matibabu ya magonjwa ya figo huko katika Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, pamoja na kukabidhi boti za uvuvi, za mwani na vifaa vya mwani kwa walima wa zao hilo.
Aidha, alikaguwa mradi wa uimarishaji wa bandari ya Mkoani ambapo Mkandarasi wa ujenzi wa bandari hiyo, China Railway Major Bridge Engineering Group ya Dar es Salaam itafanya matengenezo ya gati pamoja na nguzo za kufungia vyombo vinavyotia nanga katika bandari hiyo.
Hata hivyo, kampuni hiyo itafanya utanuzi wa kupitia vyombo vya moto na ujenzi wa njia ya abiria wa kupitia kwa miguu , ujenzi wa kuwekea makontena na ukuta wa kuzuia mmong'onyoko wa maji ya bahari.