NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba wakati umefika wa kuundwa Kamati Maalum ya Baraza la Vyama vya Siasa na kujadili masuala maalum yanayohusu Zanzibar.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo wakati akizindua kikao cha dharura cha Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, huko hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni Zanzibar.
Amesema kwamba, kwa vile chombo hicho ni cha Muungano lakini bado yapo mambo yanatofautiana kisheria baina ya pande mbili za Muuungano na kutolea mfano Sheria ya Tume ya Uchaguzi ambapo kuna sheria mbili ile ya Zanzibar ina ile ya Tanzania Bara.
Hivyo, amesema kwamba kuchanganywa kwa mambo hayo kunapelekea baadhi ya mambo kutofanywa vizuri kutokana na changamoto hiyo ya kuwa na sheria tofauti.

Aidha, amesema kwamba licha ya mafanikio yaliyopatikana tokea mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa urejee nchini mwaka 1992 pia, kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo baraza hilo limeweza kuviweka vyama vya siasa pamoja mara kwa mara katika kuzijadili changamoto na kutafuta ufumbuzi.

Alifahamisha kwamba, Watanzania wana wajibu na haki ya kujipongeza kwa kutimiza miaka 30 tokea mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa urejee tena mwaka 1992 ambapo mfumo huo bado unaendelea kuimarika hapa Tanzania kwa amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Pia, Rais Dkt.Mwinyi alieleza wajibu wa Baraza la Vyama vya Siasa kutekeleza masuala muhimu yakiwemo kuwa ni chombo kikubwa cha siasa kuhakikisha viongozi wakuu wa vyama vya siasa wanashiriki vikao vya baraza hilo, likutane mara kwa mara, kulinda tunu za taifa pamoja na kujadili na kukemea watu wanaofanya vitendo vinavyolenga kuvunja amani, utulivu na umoja wa nchini.

Rais Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anazofanya za kukuza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
Alisema kuwa,Rais Samia amekuwa akitumia njia mbalimbali ikiwemo kuleta maridhiano ya kisiasa ambapo mnamo Julai 15, 2022 alikuwa Pemba ambako alifanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa wanaoishi huko ambapo hata yeye amekuwa akikutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa nyakati tofauti na kubadilishana nao mawazo kuhusu kudumisha demokrasia, amani na umoja wa Taifa hili.
“Mimi ni muumini mkubwa wa maridhiano ya kisiasa yenye lengo la kuleta umoja wa kitaifa hivyo, navionmba vyama vya kisiasa kutuunga mkono kwa kuonesha nia thabiti ya ushirkiano wa kujenga nchi yetu,”amesema Dkt.Mwinyi.

Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ni miongoni mwa wajumbe wa kikao cha siku mbili cha zarura cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichofunguliwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) katika ukumbi wa Madinat Al Bahr Hotel nje ya Jiji la Zanzibar.
Rais Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kujali na kutekeleza masuala ya haki za wanawake ikiwemo usawa wa jinsia.
Amesema kwamba, ni ukweli usiopingika kwamba wanawake ni wadaui muhimu katika siasa za Tanzania na kueleza kwamba jambo hilo walilolifanya ni jema na wanapaswa kuliendeleza ili kuhakikisha Baraza la Vyama vya Siasa linakuwa na uwiano mzuri wa idadi ya wanawake na wanaume.
Pia, alimpongeza Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Professa Rwekaza Mukandara na timu yake kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.
Rais Dkt.Mwinyi alikumbusha kwamba chimbuko la Baraza la Vyama vya Siasa ni Zanzibar kwani Baraza la Vyama vya Siasa linatokana na muwafaka wa vyama vya siasa vya CCM na CUF uliofanyika mnamo mwaka 2001.
Alisema kuwa, hapo mwanzo baraza hilo lilikuwa halitambuliki lakini katika marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa yaliyofanyika mwaka 2009, baraza hilo likatambuliwa rasmi kuwa ni chombo cha kisheria ambacho kinaendeleshwa kwa mujibu wa sheria za nchi na uendeshaji wake unagharamiwa kwa fedha za umma.
Ametoa wito kwa vyama vyote vya siasa kulitumia baraza hilo katika kukuza demokrasia ya vyama vingi vya siasa pamoja na kulitumia kwa madhumuni ya kukuza na kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa hapa nchini.
Alieleza kwamba tokea kuanzishwa kwa Baraza la vyama vya Siasa, kumekuwa na mafanikio makubwa ya kisiasa hapa nchini kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma alitoa pongezi kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa kuanza vizuri utekelezaji wa kazi zake katika kuwaletea maendeleo wananchi, huku akimpongeza kwa kupata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.

Naye Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi alisema kuwa miongoni mwa ajenda ya kikao hicho ni pamoja na kujadili mustakabali wa vyama vya siasa nchini, kujadili hotuba ya mgeni rasmi, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na mengineyo.
Alisema kwamba jumla ya vyama 19 vimeshiriki katika kikao hicho na kueleza kwamba kwa vile chombo hicho ni cha Muungano hivyo vikao vyake vinatakiwa kufanyika katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib alieleza kwamba baraza hilo lipo pamoja na Rais Dkt.Mwinyi na kuahidi kufanya kazi nae pamoja.

Alieleza kwamba tayari baraza hilo limefuata agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na agizo la Rais Dkt. Hussein Mwinyi la kuwashirikisha kikamilifu wanawake ambapo katika mkutano huo kila chama kilikuwa na mwakilishi mwanamke.