NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kufanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha walioungana.
Mheshimiwa Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Julai 2,2022 huku akielezea kuwa, hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Serikali kuboresha matibabu ya kibingwa nchini.
"Nawapongeza Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kufanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha walioungana. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mpango wa serikali kuboresha matibabu ya kibingwa. Nawaombea watoto Rehema na Neema wapone haraka,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.
Pongezi hizo zinakuja baada tya Madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha walioungana kifuani Rehema na Neema.
Upasuaji huo uliodumu kwa saa saba, ulioanza saa 3 asubuhi na kumalizika saa 9 alasiri, ulifanikiwa licha ya ugumu na changamoto kubwa kwa watoto hao kuungana ini, moyo na baadhi ya tishu za ndani.
Aidha,upasuaji huo uliofanyika kwa mafanikio umefanyika Julai Mosi, 2022 kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Tanzania na Ireland ambao wanatokea Shirika la Operation Child Life.
Daktari bingwa wa upasuaji watoto hospitalini hapo, Zaitun Bokhari amesema, upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji watoto wadogo 12.
“Madaktari wa usingizi sita, madaktari wa kutengeneza ngozi ‘plastic surgery’ wanne, madaktari ambao kazi yao kuangalia mfumo mzima wa watoto unakwenda vizuri wawili na wauguzi sita,” amesema.
Kufanyika kwa upasuaji huo unaandika historia nyingine kwa kuwa Tanzania inakuwa nchi ya tatu baada ya Misri na Afrika Kusini katika Bara la Afrika kufanya upasuaji mgumu zaidi kwa pacha walioungana.