NA FRESHA KINASA
ZAIDI ya kata sita katika Jimbo la Mwibara Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara zinatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 6 jambo ambalo litaondoa tatizo la maji katika kata hizo na kuwapa neeema wananchi ya kupata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi wa Kata ya Kisorya jimboni humo, Mbunge wa Jimbo la Mwibara,Charles Kajege amesema kuwa, tayari serikali imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 927 kwa ajili ya upembuzi wa awali.
Amesema kuwa, kwa kipindi cha muda mrefu wananchi wamekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kitendo ambacho kilimpelekea kujenga hoja kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na tayari ndani ya muda mfupi matunda yameanza kuonekana.
Mheshimiwa Kajege amesema kuwa, mradi huo unatarajia kwenda kilometa 12 upande wa kushoto na kulia na vijiji vyote vilivyoko ndani ya kilometa hizo vitapata maji safi na salama kama ambavyo Serikali imedhamiria kuimarisha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wake na kuwezesha kumtua mama ndoo kichwani.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Nyanyama Hamisi mkazi wa Kata ya Kisorya amempongeza Mbunge wa jimbo hilo,Charles Kajege kwa kuwakumbuka wananchi wake kwani upatikanaji wa huduma bora maji ya maji safi na salama utapunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama yakiwemo amiba na homa ya matumbo (typhoid).
Hamis ameongeza kuwa, ni jambo la faraja na kufurahisha kwani Mbunge Kajege amekuwa akiwawakilisha vyema wananchi wa jimbo hilo kwa kuziwakilisha changamoto zao kwa Serikali na kwamba Serikali imeendelea kuzifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wananchi wa jimbo hilo. Huku pia akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za maendeleo zinazotekeleza miradi ya kijamii ikiwemo miradi ya maji.