Rais Samia apongezwa kwa kuagiza maboresho vyombo vya dola

NA MWANDISHI WETU

AMIRI Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan, amepongezwa ndani na nje ya nchi kwa uamuzi wake wa kuagiza mageuzi makubwa kwenye majeshi ya ulinzi na usalama nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuimarisha haki jinai nchini.Rais Samia atoa salamu za Krismasi, Mwaka Mpya
Katika mageuzi hayo makubwa yatakayoanza kwenye Jeshi la Polisi Tanzania, muundo wa majeshi hayo itapitiwa upya, ikiwemo mfumo wa ajira, mafunzo, maadili na upandishaji vyeo.

Mahusiano ya vyombo vya dola na wananchi yataangaliwa upya, ikiwemo utoaji wa haki kwa wananchi.

Rais Samia, ambaye wiki ijayo amefanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi la Tanzania, ameahidi kufanya mabadiliko makubwa zaidi kwenye jeshi hilo baada ya kupokea mapendekezo ya kamati aliyounda kupitia upya mundo wa vyombo vya dola nchini.

"Tutaanza na Polisi, wakimaliza wakileta ripoti tutafanya marekebisho halafu tunakwenda majeshi mengine," alisema Rais Samia wakati wa uapisho wa Inspekta Jenerali wa Polisi mpya, Camillus Wambura.

"Serikali sasa tunakuja na jicho jingine ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania."

Rais ameunda kamati ya watu 12 na Sekreterieti ya watu 5 kufanya kazi hiyo ya kupitia mifumo na utendaji wa vyombo vya dola, itakayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohammed Chande (Mwenyekiti) na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue (Makamu Mwenyekiti).

"Nimeunda kamati kushauri njia bora ya kuleta mabadiliko ya Utendaji kazi wenye matokeo bora kwenye vyombo vya haki ya jinai," alisisitiza.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia ameagiza ufanyike mchujo kwenye vyombo vya dola ili kubaini wenye vyeti feki na waliopewa nafasi kwenye majeshi pasipokuwa na uwezo stahiki.

"Vitendo vinafypfanyoka barabarani na polisi hudhani kuwa kweli wamehitimu masomo," alisema Rais Samia.

Taasisi nyingine za haki ya jinai ambazo zitamulikwa kwenye mageuzi ya Rais Samia baada ya jeshi la polisi ni pamoja na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Nyingine ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Jeshi la Magereza na majeshi mengine ya ulinzi na usalama.

Pongezi zamiminika ndani, nje ya nchi

Uamuzi ya Amri Jeshi Mkuu Rais Samia ya kuvifumua vyombo vya ulinzi na usalama nchini umepongezwa na wadau mbalimbali nje na ndani ya nchi

Balozi wa zamani wa Norway nchini Tanzania, Bi Hanne-Maria Kaarstad, amesema uamuzi wa Rais Samia kufanya mageuzi kwenye vyombo vya dola nchini ni jambo la muhimu sana.

Pia amepongeza uteuzi wa Jaji Chande na Balozi Sefue kuongoza kamati hiyo ya kupendekeza mageuzi hayo, akisema kuwa watumishi hao wa umma waandamizi wastaafu wana weledi mkubwa.

Semkae Kilonzo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Policy Forum, amesema uamuzi huo ni hatua nzuri.

"Hawa watu wawili (Jaji Chande na Balozi Sefue) ni wabobezi kwenye maeneo yao. Uadilifu wao unawazidi wengi waliopitia nafasi hizo," Kilonzo alisema.

"Kama wateule werevu wa Rais waliopo sasa wamesoma alama za nyakati, Rais ana malengo ya kuleta mageuzi mapana."

Naye Amne Suedi, mwanasheria binafsi, amesema kuwa ana matarajio kuwa timu iliyoundwa na Rais Samia Italeta mageuzi ya haki jinai nchini.

Mwanasheria mwingine, Deogratias Melkior Njau, amesema kuwa tangu Rais Samia aingie kwenye madaraka amechukua hatua kadhaa zinazoonesha nia ya dhati ya kujenga upya misingi ya utawala bora Tanzania.

Getrude Mollel, mtaalamu wa masuala ya mawasiliano, amesema kuwa Rais Samia anaipeleka nchi njia sahihi kwa kutoa kipaumbele kwa masuala ya haki jinai.

"Jeshi la Polisi limekumbwa na tuhuma nyingi za rushwa na matumizi ya madaraka kinyume na sheria, mambo ambayo yamechafua taswira ya jeshi hilo," alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news