Rais Samia: Hatuwezi kwenda peke yetu, lazima tushirikiane na sekta binafsi nchini

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kuna umuhimu kwa viongozi na watendaji wa Serikali kutathimini utekelezaji wa mkakati wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kuhakikisha lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote linafikiwa. 
Viongozi mbalimbali pamoja na Wageni Waalikwa wakiwa kwenye maadhimisho ya pili ya Kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa yaliyofanyika katika hotel ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 14 Julai, 2022.

Mheshimiwa Samia amesema hayo Julai 14, 2022 katika Kongamano la Pili la Kumbukizi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu , Hayati William Benjamin Mkapa lililofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar. 

Amesema ni mwaka mmoja sasa tangu uzinduzi wa mkakati huo kufanyika, hivyo kuna umuhimu kwa viongozi na watendaji serikalini kutathimini wapi azma hiyo imefikia, akibainisha haja ya kujiuliza utekelezaji wa mkakati huo, iwapo maneno yanaendana na matendo. 

Amesema kumekuwa na taarifa mara kadhaa kuwa watendaji hao wa Serikali hufuatwa na watendaji kutoka sekta binafsi, lakini matokeo yake ni kuwazungusha hadi kufikia hatua ya kukata tamaa. 

“Je? Yale tunayoyasema midomoni ya kufanyakazi na sekta binafsi, lini tutayatekeleza, baadhi yetu bado tumeelemewa na kasumba,”amesema. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wageni waalikwa kwenye maadhimisho ya pili ya Kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa yaliyofanyika Katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 14 Julai, 2022.

Hata hivyo, Rais Samia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na sekta binafsi katika hatua ya kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote. 

Akigusia Kauli mbiu ya Kongamano hilo isemayo “Ushupavu na Uongozi, chachu ya mabadiliko”,Rais Samia amesema, Watanzania hawana budi kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi endapo wanahitaji kwenda kwa kasi na kufikia lengo la Afya Bora kwa wote ifikapo mwaka 2030. 

Alieleza kuwa, bado dhana ya kuwa sekta binafsi ni mshirika muhimu katika maendeleo haijaaminika na kusema kuwa Dunia ya sasa ni ya uchumi wa soko inayoendeshwa kwa ubia, hivyo Serikali itashirikiana na sekta binafsi ili kufikia lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote. 

Aidha, aliwataka watendaji kutoka sekta binafsi kuzingatia kuwa Afya ni huduma na sio biashara. 

Katika hatua nyingine,Rais Samia amempongeza Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chisano na mwenzake wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki kwa ushirki wao katika kumbukizi hiyo, akibainisha urafiki wao wa muda mrefu na Hayati Mkapa, ambapo pamoja na mambo mengine walishirikiana katika suala la kulinda maslahi ya mataifa ya ukanda huo. 

Amesema, uwepo waokatika hafla hiyo umeiondelea hadhara hiyo upweke na kujihisi kuwa uko pamoja na Hayati Mkapa. 

Aidha, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kwa kukubali kuvaa viatu vya Mtangulizi wake (hayati Benjamin Mkapa) na kushika wadhifa wa ‘Msarifu wa Taasisi hiyo ya Benjamin Mkapa Foundation’. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapa tuzo madaktari mara baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya pili ya Kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 14 Julai, 2022. 

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imeamua kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi kwa kutambua kuwa mageuzi kama ilivyo kwa Mapinduzi, huja na mafanikio na changamoto zake. 

Amesema, atahakikisha viongozi wa Serikali wanakuwa na uvumilivu na ushupavu katika kufanikisha malengo ya kuishirikisha sekta binafsi. 

Dkt.Mwinyi amemueleza Hayati Benjamin Mkapa kuwa alikuwa kiongozi shupavu kama ilivyokuwa kwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Karume. 

Alitumia fursa hiyo kuipongeza sekta binafsi kwa kuwa na mashirikiano makuwa na serikali na kusaidia katika nyanja mbali mbali katika sekta ya Afya, hususan katika mapambano dhidi ya Maradhi ya Covid-19. 

Aidha, aliipongeza ‘Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation’ kwa kushirikiana na Serikali katika kusaidia uimarishaji wa sekta ya Afya, ambapo hivi sasa inalenga katika uanzishaji wa Bima ya Afya nchini. 

Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wale wote waliochangia katika Harambee ya kuchangisha fedha iliofanyika Hoteli ya Madinat Bahr kwa ajili ya uendeshaji wa taasisi hiyo na kusema kiasi cha shilingi Bilioni 1.2 zimepatikana ikiwemo ahadi. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais Mstaafu wa Msumbiji Joaquim Chissano mara baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya pili ya Kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa tarehe 14 Julai, 2022. 

Mapema, Rais Mstaafu Joakim Chissano wa Msumbiji alisema alimfahamu Hayati Benjamin Mkapa tangu mnamo mwaka 1966 na kumsifia kuwa alikuwa Mwandishi wa Habari mahiri (mhariri) , mwenye uwezo mkubwa wa kuchambua mambo na uwezo mkubwa wa kusikiliza. 

Anasema wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Hayati Mkapa alishirki kikamifu katika masuala ya Ukombozi wa nchi mbali mbali Kusini mwa Bara la Afrika. 

Aidha, alimsifia kuwa ni Kiongozi aliejimbanua waziwazi na bila khofu, hususan katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na kubainisha ushupavu mkubwa alionao, ambao baadae umerithiwa na Marais waliofuatia, akiwemo Mama Samia. 

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alimsifia Hayati Benjamin Mkapa kuwa katika kipindi chake cha ungozi alitoa mchango mkubwa katika utafutaji wa amani katika nchi mbali mbali Barani Afrika. 

Vile vile, alisema alikuwa na mashirikiano makubwa na Marais wa Ukanda huo, hatua iliopelekea kuanzishwa kwa Kamisheni ya Marais ya uchumi. 

Aidha, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright alisema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuhakikisha Afya kwa wote inafikiwa kupitia mashirikiano kati ya sekta binafsi na Sekta umma. 

Alisisitiza haja ya kuongeza ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya nchini. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya kumbukumbu na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Msumbiji Joaquim Chissano pamoja na Wenza wa viongozi mara baada ya maadhimisho ya pili ya Kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa tarehe 14 Julai, 2022. (Picha na Ikulu).

Kongamano hilo liliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Kitaifa na kutoka nje ya nchi, akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango, Makamo wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilali, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanziba Othman Masoud Othman. 

Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, wake wa viongozi wakuu, Mawaziri, Mabalozi, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa dini pamoja viongozi wa vyama vya siasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news