RC Makongoro Nyerere: Rais Samia amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa kwa nia njema, lakini mimi ndugu yenu nimenusurika

NA DIRAMAKINI

SAA chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya,kuhamisha wengine, kuacha na kutengua teuzi,Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Makongoro Nyerere amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuendelea kuhudumu katika mkoa huo.
Mheshimiwa Makongoro ameyasema hayo leo Julai 28,2022 wakati wa zaiara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mheshimiwa Innocent Bashungwa wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari Matui wilayani Kiteto.

"Rais (Samia Suluhu Hassan) amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa kwa nia njema, lakini mimi ndugu yenu nimenusurika, kama ningeondolewa ningesikitika maana ndio kwanza nimeanza kuwazoea,"amesema.

Uteuzi huo umetangaza leo Julai 28, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imewataja wakuu wa mikoa wapya ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Nurdin Babu ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fatma Mwasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Rais Samia pia amemteua Halima Dendego kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk t. Raphael Chegeni ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Peter Serukamba ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Pia Rais amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Kanali Ahmed Ahmed kuwa Mkuu wa Mkoa Mtwara, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Kanali Laban Thomas kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza Rais Samia amemteua Albert Chalamila kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt. Yahaya Nawanda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Waliohamishwa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza wakuu wa mikoa waliohamishwa vituo vya kazi ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa Rukwa.

Pia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe,aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Wanaoendelea

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia amewabakiza wakuu wa mikoa 10 kwenye vituo vyao vya kazi akiwemo Amos Makalla Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwingine ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batilda Burian na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Walioachwa

Wakati huo huo, Rais Samia amewaacha wakuu wa mikoa tisa akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news