NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania umesema tangu ilipozinduliwa filamu ya Royal Tour na Rais Samia Samia Suluhu Hassan idadi ya watalii wanaotembelea utalii wa Ikolojia imeongezeka kutoka watalii 49,000 kwa mwaka hadi kufikia 150,000.

Hayo yameelezwa leo Julai na Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji Utalii katika Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, (TFS) Anna Lauwo wakati washiriki wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa walipotembelea Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia kutangaza sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani.

"Ongezeko ni kubwa sana na katika kipindi kifupi, kwa hiyo unaona hii Royal Tour imehamasisha wengi kufahamu kumbe kuna utalii, kumbe Tanzania kuna kitu cha pekee ambacho sehemu nyingine hakipo na watu wameamka kumbe kuna umuhimu wa kwenda kupumzika, "amesema Lauwo.
.jpeg)
Kuhusu Msitu wa Pugu amesema msitu huo uko wilayani Kisarawe Kanda ya Mashariki na ni msitu ni moja kati ya Misitu 23 inayosimamiwa na TFS ambayo imepandishwa hadhi kutoka Misitu ya asili na kuwa msitu wa Mazingira asilia kutokana na uwepo wa viumbe na mimea adimu ndani ya Misitu hiyo ambavyo havupatikani maeneo mengine ulimwenguni.

Pia amesema kuna utalii mwingine unaofanyika kwenye mashamba ya miti yanayosamiwa na TFS akitokea mfano utalii wa kuendesha baiskeli, mazuri kwa mbio za farasi na kutembea kwa miguu msituni.

"Katika hii misitu yetu tunayofanya utalii Ikilojia haturuhusu kufanya shughuli nyingine yoyote isipokuwa utalii Ikilojia,utafiti pamoja na mafunzo na ndani ya hii Misitu tunahimiza sana uhifadhi wa mazingira kwasababu ndio kivutio kikubwa na hakuna kuangusha aina yoyote ya takataka wala kuchukua mdudu au mmea wa aina yoyote.

Pamoja na hayo Lauwo wamewahimiza Watanzania watembelee msitu wa Hifadhi ya mazingira Pugu Kazimzumbwi ambao uko karibu kabisa na Dar es Salaam, unaweza kwenda na kurudi lakini ukitaka kulala yako maeneo ya malazi.
Akielezea faida za Msitu wa Pugu mbali ya utalii amesema kuna hewa safi kabisa ambayo Dar es Salaam huwezi kuipata."Msitu huu tunasema ni mapafu ya Dar es Salaam,na tunafahamu kwa sasa hivi tunasema hali ya hewa imebadlika sana.
Hayo yote ni mabadiliko ya tabianchi lakini kuifanya hewa irudi kama awali tunahimiza uhifadhi wa misitu.Kwasababu Msitu wenyewe kama ulivyo unavuta hewa chafu na kutoa hewa safi ndio maana tunaita mapafu ya Dar es Salaam."
Kuhusu viingilio amesema mtu mzima ni Sh.2000 lakini wenye umri wa miaka sita hadi miaka 17 ni Sh.1000 na walio na umri kuanzia miaka mitano kushuka chini ni bure.