Serikali yakoleza kasi maboresho miundombinu ya viwanja vya michezo shuleni

NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI

SERIKALI inaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo kwa kuendelea kutoa fedha kujenga na kuboresha viwanja katika shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni kutambua umuhimu wa somo la michezo na kuendelea kuibua vipaji kwa wanafunzi ikiwa ni nyenzo mojawapo ya kumfanya mwanafunzi kupenda kusoma.
Sambamba na kumjenga kiafya na kumjenga afanye vizuri katika masomo lakini pia kuibua vipaji vya wachezaji wazuri na bora katika kuiwakilisha nchi katika michezo mbalimbali.
Hayo yameyasema Julai 22, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian wakati akikagua viwanja vinavyoendelea kujengwa na vingine vinavyoendelea kufanyiwa ukarabati katika Shule ya Sekondari Tabora Boys na Girls kwa ajili ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Mashindano ya Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA).

Dkt. Batilda amesema, pamoja na maendeleo mazuri yanayoendelea katika ujenzi huo amewataka wasimamizi na mafundi kuzingatia muda, ubora na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali katika uwekezaji wa ujenzi wa viwanja hivyo na kusema si tu vitatumika kwa michezo hiyo bali ni viwanja endelevu vitakavyoendelea kutumika kizazi hadi kizazi.
“Ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu katika michezo sisi viongozi tutaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo inayoletwa kwa kuhakikisha tunaisimamia kwa ubora unaotakiwa," amesema Dkt. Batilda

Ameendelea kueleza namna mkoa ulivyojipanga kwa kupokea wageni wote na kuwahakikishia mahitaji muhimu yote yapo na yanapatikana na kuahidi kutoa ushirikiano na viongozi wote wa Mkoa wa Tabora wapo tayari kupokea mashindano hayo ambayo yatafanyika Kitaifakoa huo.

“Nitoe wito kwa wenyeji wenzangu tufanye kazi kwa kujituma na kwa amani ugeni huu utatusaidia kuongeza kipato endapo tu tutajituma kwa kufanya biashara zetu za kihalali na amani tuboreshe biashara kama mnavyofahamu Tabora hatuna jambo dogo,”amesema.

Kwa upande wa Afisa Elimu Mkoa, Mwalimu Juma Kaponda ameishukuru Serikali kwa mashindano hayo kupendekezwa kufanyika Mkoa huo amesema, washiriki wenyeji wapo tayari kushiriki na kufanya vizuri kwa sababu wamekua wakiendelea ufanya mazoezi amesema, kuwepo kwa mashindano hayo katika Mkoa wa Tabora wataendelea kujituma kwa kufanya vizuri zaidi.

Naye Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. George Mbijima amesema, maandalizi yapo vizuri na yamekamilika na kwa upande wa shiriki 3900 UMITASHUMTA na 4200 UMISETA amesema, jumla hiyo ni pamoja viongozi wa wanamichezo hao.

Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa michezo kuonesha vipaji vyao kwa kuzingatia sheria na taratibu za michezo kutoka kwa walimu kwani michezo ina sheria zake kama ilivyo katika masomo mengine.
"Tuoneshe vipaji kwa kufanya vizuri michezo imezingatiwa makundi yote ikiwemo kundi la watoto wenye mahitaji maalumu,"amesema Mbijima.

Jumla ya Mikoa yote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar itashiriki michezo hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news