NA SAID MWISHEHE
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani Pemba huku akitumia nafasi hiyo kueleza Chama hicho kitaendelea kuwalinda na kutambua mchango wa wabunge,madiwani na wawakilishi ambao wako mstari wa mbele kutekeleza miradi ya maendeleo.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka (wa pili kulia) akikabidhi funguo ya gari la kubebea wagonjwa kwa mmoja ya wananchi wa Jimbo la Gando (wa pili kushoto). Shaka amekabidhi funguo za gari hilo jana likiwa limetolewa na Mbunge wa Jimbo la Gando, Salim Mussa Omari (wa kwanza kushoto) na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa.
"Utekelezaji wa miradi unaofanywa na viongozi wa CCM unalenga kutekeleza ahadi na kutatua changamoto za wananchi katika huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji.Niwahakikishie wabunge,madiwani na wawakilishi wanaotokana na CCM kwamba Chama kitaendelea kuwalinda dhidi ya yeyote anayetaka kuwavuruga na kusababisha washindwe kutekeleza majukumu yao.

"Wabunge,madiwani na Wawakilishi wanapaswa kuachwa watekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba mwanachama yeyote mwenye malengo ya kuomba uongozi asubiri wakati mwafaka unaoruhusiwa kisheria,"amesema Shaka .
Maelezo hayo ya Shaka yalitokana na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Gando kutoa kilio chao mbele ya mkutano huo kuna baadhi ya wanachama wa Chama chao wamekuwa wakiwashika mashati na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu pamoja na miradi ya maendeleo,hivyo kutoa ombi kwa Chama kuangalia namna ya kukomesha hali hiyo.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (katikati) akisalimiana na Mwananchi wa jimbo la Gando vsiwani Pemba baada ya kumkabidhi baiskeli ya Kutembelea iliyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo Salim Mussa Omari (wa pili kulia). Shaka amemkabidhi baiskeli hiyo jana na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa.
Awali kabla ya kuhudhuria mkutano huo mapema asubuhi aada ya kuwasili kisiwani Pemba , Shaka alizuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu marehemu Dk. Omari Ali Juma, wilayani Chakechake.
Shaka baadae alikwenda kwenye kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar marehemu Maalim Seif Sharif Hamad lililopo Kijiji cha Mnyali, Mtambwe wilaya ya Were Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akiwa katika makaburi hayo Shaka ametumia nafasi hiyo kueleza mchango wa viongozi hao ambao enzi za uhai wao wamelitumikia Taifa kwa uadilifu mkubwa na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akiwa sambamba na Mbunge jimbo la Gando Mhe.Salim Mussa Omari (wa pili kulia) akishiriki ujenzi wa kisima cha maji safi na salama katika Jimbo la Gando, miradi ambayo imewapunguzia adha wananchi ikiwemo ya kufuata maji umbali mrefu.
Aidha amesema wakati Watanzania wakiwa wametimiza miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa mchango wa Dk .Omari Ali Juma pamoja na Maalim Seif hautasahaulika kwani walijitoa kwa kiwango kikubwa kuufanikinisha mfumo huo.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akishiriki ujenzi wa kisima cha maji safi na salama katika Jimbo la Gando, miradi ambayo imewapunguzia adha wananchi ikiwemo ya kufuata maji umbali mrefu.