Spika Dkt.Tulia:Tufungamanishe sekta za kilimo na nishati ukanda wa SADC

NA DIRAMAKINI

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Tulia Ackson ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufungamanisha sekta za kilimo na nishati kupitia mikakati mbalimbali ya kukuza uchumi inayotekelezwa kwenye nchi hizo.
Akizungumza Julai 13, 2022 katika Mkutano Mkuu wa 51 wa Jukwaa la Mabunge ya SADC, unaoendelea jijini Lilongwe nchini Malawi, Dkt. Tulia amebainisha umuhimu wa kufungamanisha sekta hizo ili ziwezeshe ukuaji wa uchumi katika ukanda wa SADC.

“Endapo tunahitaji nchi zetu ziweze kujitegemea kwenye suala la usalama wa chakula, tunapaswa kujifunza kupitia nchi zingine zilizofanikiwa katika sekta hii kama zilivyoainishwa kwenye taarifa ya kamati ya chakula.

“Tunapaswa kuweka kipaumbele kwenye miundombinu wezeshi itakayosaidia kukuza sekta ya kilimo, kama ni sekta ya nishati basi twende pamoja kama Jumuiya kuhakikisha inakuza kilimo chetu,” amesema Dkt.Tulia.

Akitolea mfano nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Spika amesema, “Nakubaliana na wenzetu wa Kongo kuwa mradi wa umeme wa maji wa Inga unaweza kutoa umeme kwa nchi zote za SADCna hivyo kusaidia katika juhudi za kukuza sekta ya kilimo.”

Dkt. Tulia amewaomba wajumbe wa Mkutano huo kuweka nguvu kwenye maeneo mengine ya kiuchumi yatakayofungamanishwa ili kukuza sekta ya kilimo kabla ya kufikiria kupata wawekezaji wakubwa watakaokuja kuwekeza katika sekta hiyo. 

Aidha, Dkt. Tulia ametoa wito kwa wajumbe hao kuzishauri nchi zao kuondoa vikwazo katika biashara ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwa wingi miongoni mwa nchi hizo kama sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya kilimo. Kadhalika, Mhe.Spika ameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa biashara baina ya nchi hizo ili kuhakikisha kunakuwapo na soko la uhakika kwa mazao yanayozalishwa na wakulima.

“Iwapo nchi mojawapo katika ukanda huu inazalisha kwa wingi zao fulani, kwanini nchi zingine wanachama zisiiunge mkono kwa kununua zao hilo badala ya kwenda kununua katika nchi zilizo nje ya Jumuiya ya SADC,kwa kufanya hivyo tutatengeneza soko la ndani la bidhaa za kilimo,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news