NA MATHIAS CANAL-WEST
SERIKALI ya Tanzania na Afrika Kusini zinarajiwa kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya elimu msingi Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai ambapo kitaifa yatafanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 4 Julai 2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini Mhe Matsie Angelina Motshekga katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya Mazungumzo hayo Waziri Mkenda amesema kuwa mkataba huo wa makubaliano unasainiwa ikiwa ni kutekeleza ahadi ya viongozi wakuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na Rais wa Afrika Kusini Mhe Cyril Ramaphosa waliyoitoa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.

Waziri huyo wa Elimu wa Afrika Kusini anatazamiwa tarehe 5 Julai 2022 kutembelea shule ya msingi ya Uhuru Mchanganyiko kadhalika kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Balozi Liberata Mulamula pamoja na kukutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Mussa.
