NA RESPICE SWETU
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaotekelezwa katika halmashauri zote nchini, umeleta faraja kubwa kwa watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma baada ya walemavu 944 wa aina mbalimbali kuingizwa kwenye mpango wa kunufaika na mfuko huo.
Baadhi ya walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) waliohudhuria mafunzo.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Almachus Njungani amesema, kuibuliwa kwa kundi hilo ni matokeo ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwezi Mei na Juni, mwaka huu.
Amesema, miongoni mwa kazi zilizofanyika katika kipindi hicho, ni kupita kwenye kaya za walengwa wa mpango huo kuwabaini watu wenye ulemavu na kuwaingiza katika orodha ya walengwa watakaokuwa wakinufaika na ruzuku zitokanazo na mfuko wa mpango huo.
Sanjari na kuliibua kundi hilo, Njungani amezitaja shughuli nyingine zilizofanyika katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana wenye umri wa miaka kati ya 14 na 19 kuhusu afya, utunzaji wa kumbukumbu, mifumo ya fedha na uibuaji wa miradi ya ajira za muda ambapo takribani miradi 64 ikiwemo ya maji, barabara na utunzaji wa mazingira iliibuliwa.
Akizungumzia gharama za utekelezaji wa shughuli hizo, Njungani amesema kuwa zaidi ya shilingi milioni mia moja zimetumika zikiwa ni ufadhili wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).