NA FRESHA KINASA
MWENYEKITI wa Chama cha Wafanyabiahara Kilimo na Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniphace Ndengo amesema kupitia maonesho ya Kimataifa ya Mara International Business Expo yanayotarajia kufanyika Mkoa wa Mara kuanzia Septemba 2 hadi 11, 2022 ambayo yatawakutanisha washiriki 50,000 hadi 100,000 yatachochea kuufanya Mkoa wa Mara uwe eneo jipya la uwekezaji kwa kuzitangaza fursa mbalimbali za kiuchumi kimataifa na kuchagiza maendeleo ya wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.

Maonesho ambayo yatafanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma. Ambapo yanatarajia kuufungua mkoa kiuchumi kutokana na washiriki mbalimbali watakaofika na kuziona fursa zilizopo na waweze kuzitumia kwa tija kuwekeza na hivyo kuzalisha ajira na fursa mbalimbali ambazo zitaleta mchango mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
"TCCIA Mkoa wa Mara inakusudia kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara mbalimbali duniani ili kuwaambia uzuri wa mkoa na kwamba wakiwekeza watapata tija kubwa kiuchumi na kuwanufaisha pia wana Mara kiuchumi kupitia sekta muhimu za uzalishaji za viwanda, biashara, kilimo bora na kutumia uwepo wa Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuchochea uchumi wa mkoa na taifa letu," amesema Ndengo.
"Maonesho haya yatawakutanisha pia wafanyabiashara wengi kutoka mataifa mbalimbali na yataleta muingiliano wa watu wakiwemo wajasiriamali wadogo, makampuni, sekta za umma na mashirika,, wafanyabiashara wakubwa tunatarajia baada ya maonesho kutakuwa na makongamano na majukwaa mbalimbali yatafanyika kuja kuonesha jinsi gani mkoa sasa unaendelea. Sambamba na kupunguza migogoro Kati ya wawekezaji na Wananchi ili kujenga mahusiano bora na habari kubwa iwe ukuzaji wa biashara na Viwanda katika Mkoa wetu,"amesema Ndengo.
Aidha amesema, katika maonesho hayo chemba mbalimbali za wafanyabiashara zimealikwa kutoka Uganda, Kenya, Kongo, Burundi na zimesema zitaleta washiriki.


Awali Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara,Dkt.Noel Crispine amesema, maonesho hayo pia yatawezesha kuwatangaza wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara na wajasiramali pamoja na bidhaa zao sambamba na kutangaza vivutio mbalimbali na fursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo kwa wafanyabiashara na makampuni ya kigeni yatakayoshiriki katika maonesho hayo na kujenga ushirikiano mzuri wa kibiashara miongoni mwao.
Ameongeza kuwa, Mkoa wa Mara umeandaa mwongozo unaoainisha fursa zilizopo ikiwemo sekta ya utalii, kilimo, viwanda na kwamba mkoa umebarikiwa kuwa na fursa ya Hifadhi ya Serengeti na Ziwa Victoria. Hivyo kazi ya serikali ni kutafsiri fursa hizo ili ziwaletee maendeleo wananchi na kwamba, sekta binafsi ni muhimu ikashirikishwa kwa upana kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani humo.

Aidha, Dkt.Noel amewataka wananchi, wajasiriamali,wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ambayo amesema yatakuwa na chachu kubwa ya kuleta mageuzi na maendeleo thabiti ndani ya Mkoa wa Mara.