NA MWANDISHI WETU
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewakaribisha wananchi na wadau wote wa uwekezaji kutembelea banda lao katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Mwalimu Nyerere Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi.Pendo Gondwe akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar-es-Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo Meneja Uhusiano na Mawasiliano, Bi. Pendo Gondwe amesema, "Kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu katika maonesho haya ya Sabasaba inayosema Tanzania mahali sahihi kwa Uwekezaji na Biashara, kwa hakika ni mahala sahihi pa uwekezaji, hivyo tunakuomba wewe mdau wa uwekezaji uweze kufika katika mabanda yetu ili uweze kujifunza masuala mbalimbali ya Uwekezaji. Tunapatikana katika Banda namba 14 PTA na jengo la Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara,"amesema.
Amesema, majukumu ya TIC ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji, kuwahudumia wawekezaji kupitia kituo cha mahala pamoja, Kuratibu majukumu mbalimbali yahusuyo Uwekezaji na kuishauri Serikali juu ya kuboresha mazingira ya Uwekezaji na Uwekezaji kwa ujumla."