Tunafanya zaidi ya hapa kuinua vipaji vya vijana Zanzibar-Rais Dkt.Mwinyi

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba ujenzi wa viwanja vya michezo vya kisasa hapa Zanzibar utasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua vipaji kwa vijana. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiendesha gari la michezo (Ballcut) baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kiwanja cha michezo cha The Legend Sports Center kinachonjengwa katika eneo la Kombeni Kisakasaka Wilaya ya Magharibi "B" Unguja wakati wa ziara yake katika wilaya hiyo kutembelea ujenzi wa miradi ya maendeleo Julai 17, 2022.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Julai 17, 2022 baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa viwanja vya michezo unaojengwa na Kampuni ya F.L.A ya wawekezaji wazawa vilivyopo Kisakasaka, Shehia ya Kombeni Jimbo la Dimani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi. 

Katika maelezo yake Rais Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa vijana walioanzisha mradi huo wa viwanja vya michezo na kueleza hayo ndio maono yake katika suala zima la viwanja vya michezo. 

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, viwanja vinavyotakiwa kujengwa hivi sasa ni vyenye mfano kama huo ambavyo vina sifa ya kuweza kutumika usiku na mchana na vyenye mazingira mazuri. 
Alisema kwamba yeye ni muumini wa michezo na kusisitiza azma ya Serikali ya kujenga viwanja kama hivyo vya kisasa ambavyo vitakuwa vikitumika wakati wote na kuhusisha michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa ‘Go-karting’. 

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaunga mkono vijana hao ili waweze kuendesha vizuri mradi wao huo. 

Aliwapongeza viongozi wa Mkoa na Wilaya kwa usimamizi mzuri wa kuhakikisha mradi huo unafanikiwa huku akiwaahidi kwamba wateja wengi watawapata mara tu watakapoanza shughuli zao za michezo katika viwanja vyao hivyo. 

Nao viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliopata fursa ya kutoa salamu na shukurani zao walimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa maono yake ya kutaka kuimarisha viwanja vya michezo vya kisasa kama hicho alichokiwekea jiwe la msingi. 

Walitumia fursa hiyo kueleza kwamba maamuzi ya vijana hao ya kukaa pamoja na kubuni mradi huo ni wazo sahihi ambalo litaisaidia Serikali katika mikakati yake ya kuimarisha miundombinu ya michezo hapa Zanzibar. 

Viongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo walieleza jinsi walivyotoa ushirikiano wao kwa vijana hao mpaka kufikia hatua hiyo. 

Nae Msimamizi wa The Legend Sport Centre, Fahmi Moh’d Abdi alimueleza Rais Dkt.Mwinyi jinsi hatua zilivyochukuliwa katika ujenzi wa viwanja hivyo wakati akimtembeza katika eneo hilo. 
Akitoa taarifa ya ujenzi huo miongoni mwa vijana walioekeza mradi huo alisema kwamba eneo la utalii wa michezo bado unataka kuongeza nguvu kama vile michezo ya Go-Karting na kusema kwamba mradi huo utatumia shilingi Bilioni 3 hadi kumalizika kwake, ambapo hadi walipofikia wameshatumia shilingi Bilioni 1.3. 

Alieleza kwamba mradi huo una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kutoa ajira za muda 234 na baada ya kumalizika zitatoka ajira za kudumu 86 pamoja na kuchagia utekelezaji wa sera za uchumi wa buluu kimichezo na kukuza sekta ya utalii na kuongeza kodi, afya kwa jamii na kutoa burudani sambamba na kuimarisha afya. 

Alisema kuwa mradi huo una lengo la kushirikiana na Serikali katika kuimarisha vipaji vya madereva wa langalanga hasa katika kuzalisha madereva wa ‘fomular one’, ligi za mpira pamoja na ligi za gari na michezo mengine. 

Aliongeza kwamba mradi huo utasaidia kuanzisha chuo cha michezo ambacho kitasaidia kuwafundisha vijana michezo kadhaa ikiwemo kuogelea na kuleta mapinduzi ya michezo hapa Zanzibar. 

Pamoja na hayo, vijana hao walieleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao huku wakiiomba Serikali iendelee kuwaunga mkono hasa katika kupata zaidi mkopo huku wakitoa shukurani kwa kupata sehemu ya mkopo wa fedha za UVIKO-19 ambao umewasaidia katika shughuli zao za kuanzisha mradi huo. 
Walimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa sera zake nzuri ambazo zinaelekeza na kuinua uchumi wa Zanzibar na kupanua wigo wa kuongeza ajira kama alivyoahaidi katika Ilani ya CCM kwa kuahidi ajira 300,000 ambapo kwa upande wao wameahidi kutoa ajira 86 sambamba na kuwa na muono wa kuimarisha sekta ya michezo hapa Zanzibar. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news