Tunahitaji uwekezaji mkubwa, Waziri Prof.Mbarawa aieleza bodi mpya ya TBA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuuwezesha Wakala huo kuwekeza kikamilifu katika viwanja vyake vilivyopo katika maeneo ya kimkakati ili kumaliza tatizo la upungufu wa nyumba za viongozi na watumishi wa umma lililopo nchini.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimkabidhi vitendea kazi Mjumbe wa Bodi mpya ya Ushauri ya TBA, Bi. Vicky Jengo mara baada ya kuizindua Bodi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuzindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema huu ndio wakati wa TBA kujiimarisha kimiundombinu na kiuchumi kwa kutumia fursa ya mahitaji ya nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma na majengo ya kibiashara katika miji mikuu.

“..Hakikisheni mnakuja na mipango ya kutumia rasilimali ya viwanja na majengo mlio nayo kupata faida kwa kujenga majengo mazuri katika maeneo ya miji na kuhakikisha nyumba zenu zaidi ya elfu sita zilizopo zinakuwa katika viwango bora wakati wote na kuvutia wapangaji,” amesema Prof. Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati akizindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati akizindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Dar es Salaam leo, Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (Sekta ya Ujenzi), Bw. Rafael Nombo na Kaimu Mkurugenzi Huduma za Ufundi Qs. Optatus Kanyesi wakifuatilia.

Prof. Mbarawa ameipongeza TBA, kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 3,500 Nzuguni Jijini Dodoma na kuongeza kuwa mradi huo ukikamilika kwa wakati utawaongezea mapato kwa kuwa bado mahitaji ya nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo ya mijini ni makubwa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Dk. Ombeni Swai (kushoto), na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro (katikati), wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Dk. Ombeni Swai mara baada ya kuizindua Bodi hiyo, katikati ni Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro akishuhudia.

“…Tengenezeni mikakati ya ubunifu itakayo wawezesha kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha sekta ya majenzi na makazi ya viongozi na watumishi wa umma inaimarika,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Arch. Dk. Ombeni Swai amesema Bodi yake itafanya kazi kwa uadilifu na ubunifu ili kuiwezesha TBA kupata faida na kutoa huduma ya kuaminika kwa Watanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa miongozo anayoitoa na kusisitiza kuwa TBA itaendelea kusimamia mifumo, nidhamu, udhibiti na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba na majengo ya Serikali nchini kote kwa kuzingatia mahitaji na faida ili kukuza mtaji ikiwemo ujenzi wa nyumba 3,500 jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi Mpya ya Ushauri na Menejimenti ya TBA jijini Dar es Salaam

Wajumbe wapya wa Bodi ya Ushauri ya TBA itakayohudumu kwa miaka mitatu ni pamoja na Arch. Dk. Ombeni Swai (Mwenyekiti), Qs. Optatus Kanyesi (Mjumbe), Bw. Shaban Kabunga (Mjumbe), Qs. Joseph Mkali (Mjumbe), na Bi. Vicky Jengo (Mjumbe).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news