‘Tunamkumbusha Waziri wa Habari kuongeza kasi’

NA GODFREY NNKO

IMEELEZWA kuwa,kasi ya Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria za Habari nchini imepungua tofauti na ilivyotarajiwa. 
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi huku akifafanua kuwa, kasi iliyopo sasa inatia mashaka kukamilika kwa mchakato huo kabla ya Bunge la Mwezi wa Tisa.

“Hapo awali tulikwenda vizuri, lakini tangu baada ya Mei 3 mwaka huu (Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani), tunaona kasi imepungua kidogo,”amesema Balile.

Amesema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye alikuwa akisisitiza kukamilisha jambo hilo, lakini kwa sasa, kazi ya kuelekea mafanikio imepungua.

Na kwamba, hapo awali serikali kupitia Wizara ya Habari chini ya Nape, ilipanga kufanya vikao mbalimbali na wadau wa habari, lakini mpaka sasa havijafanyika.

“Tungependa kujua. Wizara ilikuwa imepanga kufanya mikutano kadhaa na kujadiliana na wataalamu wa tasnia hii, lakini sasa tunaona kama kila kitu kimesimama na tunapoendelea kuuliza, tunaambiwa bado mikutano ipo,” amesema Balile.

Balile amesema, mabadiliko ya sheria hizo bado ni muhimu kwa mazingira ya sasa huku akipendekeza kasi ya mabadiliko hayo ili kuwa Bunge la Novemba kwa kuwa ndio bunge la miswada.

“Bado tunazihitaji sheria, bado tunahitaji hayo mabadiliko haraka kadri inavyowezekana kuliko wakati wowote ule kwa sababu, tukipitwa na lile bunge la mwezi wa tisa, ina maana tutasubiri mwaka mmoja baadaye. Bunge la mwezi wa tisa ndio la miswada,”amesema.

Pamoja na kuchelewa huko, Balile amasema iwapo wizara yenye dhamana ikiamua sasa kuongeza kasi katika mchakato huo, upo uwezekano mkubwa wa kufikia malengo ndani ya muda mwafaka.

“Tunachotafuta zaidi ni haki ya kupata habari na uhuru wa vyombo vya habari. Huu uhuru unawezesha haki nyingine kupatikana. Mfano demokrasia na vingine vyote vinavyozungumzwa, vinatokana na uhuru wa watu kutoa mawazo yao.

“Inapokuwa uhuru haujalindwa kisheria, basi unachelewesha hivi vingine kupatikana katika jamii. Huu ni mjadala na mchakato tunaopaswa kushirikishana tulio wengi kwa pamoja,”amesema.

Hata hivyo, Nape akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo kusaidia ukuaji wa habari Julai 13, 2022 jijini Dar es Salaam alisema, serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuwasilisha mbadala wa maoni yao na kwamba, na ina malengo ya kuukamilisha mchakato huo kwa muda mfupi. 

“Serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa, tukae mezani tuzungumze na huo mchakato hauwezi kuwa mfupi, ni mchakato wa mazungumzo, mie nimeukuta na tunaendelea nao. Tuna malengo ya kuukamilisha mapema kadri inavyowezekana,” alisema Nape na kuongeza;

“Sheria ya habari ilipotungwa, ililenga kutatua matatizo ya habari ikiwemo ajira zao, maslahi yao, mazingira yao ya kazi, haki zao na wajibu wao. Sasa inawezekana masuluhisho yaliyopo kwenye sheria, ndio yanayogombaniwa kwamba ni sahihi ama si sahihi.”

Alisema, lengo la mchakato wa sasa ni kutengeneza sheria zitakazodumu kwa muda mrefu na ambazo zitakubalika katika pande zote mbili (serikali na wadau) pia zitakazotengeneza mazingira kuwa bora zaidi kuliko ya sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news