NA MWANDISHI WETU
UJUMBE wa wataalamu kutoka Wizara ya Elimumsingi ya Afrika Kusini umetembelea Shule ya Msingi Chief Albert Luthuli iliyopo Mazimbu mkoani Morogoro.

Akiwa shuleni hapo Mkuu wa Msafara huo, Enoch Rabotapi ambaye ni Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu nchini humo (Chief Director for Teacher Education) ameahidi ushirikiano kati ya shule hiyo na baadhi ya shule zitakazobainishwa nchini Afrika Kusini kwa kubadilishana uzoefu na walimu.


Akizungumza kabla ya kuanza ziara katika Shule hiyo Sylvia Lupembe, Mkuu wa Mawasiliano Serikalini Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema, ujumbe huo uko nchini kuungana na watalaamu wa elimu wa hapa nchini na wa Kiswahili kwa ajili kuandaa Mpangokazi wa Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika kuendeleza elimumsingi ikiwemo ufundishaji Kiswahili nchini Afrika Kusini.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chief Albert Luthuli, Theresia Swai ameishukuru nchi ya Afrika Kusini kwa kuendeleza ushirikiano na nchi Tanzania na kuthamini mchango wa nchi yetu katika harakati za ukombozi wa nchi yao.