Ukimya wa Namba 3 mkoani Mara kuchukua fomu CCM wazua maswali, watoa ya moyoni

NA MWANDISHI WETU

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na wananchi mbalimbali mkoani humo wamesema, muda wowote watafanya maandamano ya amani ili kujua iwapo Mwenyekiti wa chama hicho mkoa anayemaliza muda wake, Samuel Kiboye (Namba Tatu) anachukua fomu.

Kwa nyakati tofauti wamesema, iwapo Kiboye hatakwenda kuchukua fomu watamchukulia na kumpelekea popote alipo kwa kuwa, bado ni hitaji lao kwa ustawi wa chama na usimamizi wa Ilani ya Uchaguzi kwa manufaa ya wananchi.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi wa habari wilayani Rorya,Musoma Vijijini, Musoma Mjini,Tarime,Bunda,Serengeti na Butiama.

"NambaTatu,kazi aliyofanya ni kubwa sana katika mkoa huu wa Mara, amefanya mkoa umetulia pamoja na kumaliza makundi ndani ya chama.

"Pia amekuwa mstari wa mbele kusaidia wananchi ni mwenyekiti ambaye hata ukimpigia simu usiku anapokea tofauti na viongozi wengine ambao wako Mara, tunauliza kama hajachukua fomu tutaandamana. Na tutamchukulia kumpelekea kokote alipo, bado tunahitaji aendelee kuwajibika kwa manufaa ya chama na usimamizi wa ilani mkoani hapa,"amesema Mwita James mkazi wa Musoma.

Naye Bhoke Chacha kutoka Tarime amesema kuwa,wameshangaa kuona Namba Tatu yupo kimya kuhusu uchukuaji fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo.

"Hii si hali ya kawaida, Namba Tatu ametulia sana mpaka tumepata wasiwasi sisi kama wana CCM tunataka kujua kama mwenyekiti wetu mwenye nguvu amechukua fomu, na kama hajachukua kitu gani ambacho kinamkwamisha,"amesema Bhoke.

Naye mkazi wa Serengeti aliyejitambulisha kwa jina la Manga amesema kuwa, iwapo hawatapata sababu za msingi kabla ya Ijumaa (leo) wataandamana kujua kama amechukua fomu au bado.

"Tunachotaka kujua ni iwapo amechukua fomu au bado, Kiboye ni mpenda watu anayesema ukweli. Kama bado tutamchukilia fomu,"amesema Manga.

"Pia wameanza kampeni mapema sana, wako vigogo watatu wanajiita mamiliionea kutoka Tarime,Serengeti na Bunda,tunaomba mwenyekiti wetu Namba Tatu achukue fomu ndiye atakayekomboa Mara kwenye uchaguzi wa vitongoji na vijiji na mtaa peke yake hawa waliobaki wana maslahi yao kwenye chama.

"Pia ndiye kiongozi pekee anayemsemea Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali vizuri,wengine wanatafuta vyeo hata Rais hawamsemei kwa kazi anazofanya,tuko tayari kumchukulia fomu Namba Tatu,"wamesema kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Mwenyekiti anayemaliza muda wake CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) ili kupata ufafanuzi iwapo amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, "nipo katika maombi kwa sasa, naomba mnipe muda nitatoa taarifa kabla au baada ya Ijumma (Julai 8, 2022),"amesema Kiboye. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news