Unywaji wa juisi ya Rosella na faida tele katika afya yako

NA DIRAMAKINI 

NI wazi kuwa, wengi wetu tumekuwa tukitumia mitishamba kutibu maradhi mbalimbali, lakini siku za karibu utafiti wa sayansi unaonesha kuwa mti wa ‘hibiscus sabdarifa’, unaojulikana kama Rosella umeibua habari mpya kuwa unaweza kutibu shinikizo la damu. 
Matumizi ya dawa za miti shamba, si maarufu kwa watu barani Afrika pekee,bali hata nchi za Ulaya kama Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi na hata China. 

Umaarufu wa vituo vya kutoa huduma za afya, unaonesha namna dawa za mitishamba zinavyokubalika na zinavyotumika katika viwanda vingi vikiwamo vya vipodozi. 

Ukweli kuwa dawa hizo zinatumika, kumebainika pia kwa kuongeza gharama za matumizi ya kila siku katika kutunza afya zao na kuboresha maisha yao. 

Miongoni mwa vipodozi vinavyotokana na mitishamba ambavyo vinapendwa na watumiaji wengi ni vile vinavyotumika katika kutengeneza upya ngozi, kuondoa magamba mwilini na kutumika kama krimu ya kulainisha na kuboresha ngozi mwilini.

Dawa za mitishamba zinatumika zaidi China, India, Japan, Pakistan, Sri Lanka na Thailand. Nchini China, zaidi ya asilimia 40 ya matumizi ya dawa nchini humo ni ya mitishamba. 

Watu wengi wanaoishi mijini hawana habari juu ya utajiri wa maua na mimea inayowazunguka ambayo Mungu amewapa na ambayo ina faida kubwa katika maisha yao ya kila siku. 

Wanasayansi wanathibitisha kuwa mmea wa Rosella, unaopatikana katika maeneo mengi nchini, ni tiba muhimu ya shinikizo la damu kuanzia hatua za mwanzo hadi linapofikia hatua ya kati. 

Hadi sasa majaribio mengi yamefanyika kwa kutibu wanyama na binadamu na yameonesha mafanikio makubwa upande wa utunzaji na upunguzaji shinikizo la damu. 

Inaelezwa kuwa, maji ya miti hiyo yakikamuliwa yanakuwa na ubora sawa na dawa nyingine za hospitalini zinazotibu shinikizo la damu. 

Mfumo wa namna ya kutengeneza dawa za kushusha kiwango cha shinikizo la damu bado unahitaji kufanyiwa utafiti zaidi. 

Lakini matokeo yaliyopatikana kutokana na kutibu wanyama, yameonesha wazi kuwa mmea huo unatoa tiba salama na haujasababisha madhara kwa wanyama na binadamu. 

Pamoja na kupunguza shinikizo la damu, utengenezaji dawa kutokana na mti huo pamoja na vikonyo vya majani yanayohifadhi maua ambayo kabla hayajachanua yanasaidia kupunguza mgandamizo wa damu mwilini. 

Dawa hiyo ina kazi ya kupunguza oksijeni mwilini na inaweza pia kutumika kuzuia saratani na magonjwa kwenye maini, hasa kwa wanywaji wa pombe. 

Ni nzuri kuitumia kwa wagonjwa wa upungufu wa damu, kwani imeonesha wazi ina uwezo wa kuimarisha mfumo unaoshikilia chembechembe nyekundu za damu. 

Dawa hiyo inasaidia kuhuisha upya maisha ya mtu mwenye upungufu wa damu. Kwa upande wa chakula bora, dawa hiyo ni tajiri wa vitamani C, thiamin, riboflavin na niacin. Pia ina madini muhimu mwilini ambayo ni calcium, phosphorus na chuma.

Kwa miaka mingi, Rosella imekuwa ikitumika katika nchi mbalimbali kama nishati muhimu ya kupikia na chanzo mahususi cha dawa za kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu. 

Dawa hii ilitumika kwa wingi barani Asia, Amerika Kusini, Visiwa vya Caribbeani, Ulaya na Asia. Ilitumika katika kuandaa mishumaa, mafuta na viungo moto na baridi na ilitengeneza mvinyo mzuri wa kunywa. 

Ukichanganya na chai utajisikia unakunywa kinywaji chenye harufu nzuri inayonukia kama dawa na kama kirutubisho mwilini. 

Si ajabu kusikia dawa hiyo baada ya kunywa inaondoa uchovu, mafua na maradhi ya tumbo hasa ya kujaa gesi. 

Taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inasema, kuzuia magonjwa sumbufu, ni uwekezaji muhimu katika maisha ya binadamu.

Aidha,wataalam wa afya wanasema,mmea huu wenye virutubisho vingi kama vitamini na madini ya aina mbalimbali, ni kinga ya magonjwa mengi kama saratani na ukosefu wa lishe bora.

Faida nyingine ya Rosella ni kuongeza nguvu za kiume, inasaidia kutibu magonjwa ya tumbo, majipu, matatizo ya moyo, kikohozi na homa za mara kwa mara.

Kwa wagonjwa wenye maambuzi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) wanashauriwa watumie kwa wingi Rosella kwani,inasaidia kuongeza nguvu na damu. 

Inashauriwa, kuyachemsha kwanza maua ya Rosella kabla ya kutengenezwa juisi kwa ajili ya matumizi yako ya kila siku nyumbani.

Ukiwa mtumiaji mzuri wa Rosella tarajia kuyapa kisogo magonjwa ya shinikizo, sukari,kikohozi na mafua,kupunguza uzito wa mwili na tarajia kuwa na ngozi nzuri ya kuvutia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news