NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iko makini na haitaki mzaha katika matumizi ya fedha za umma zinazoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Manyoni mjini, wakati aliposimama kusikiliza kero zao, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida, Julai 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Ameyasema hayo Julai 15, 2022 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manyoni na Itigi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida. “Serikali yenu iko makini na Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kuwa hataki mzaha na matumizi ya fedha za umma, hakuna atakayebaki salama na hakuna mtumishi atakayeonewa.
Amesema kuna wizi mkubwa wa mapato ya Serikali kupitia mifumo ya makusanyo kwenye halmashauri nchini ikiwemo na Halmashauri ya Manyoni, hivyo ameagiza kila aliyepewa dhamana ya kusimamia Halmashauri ajipange kusimamia makusanyo pamoja na matumizi yake.
Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida Bw. Mzalendo Widege kuwahoji wakusanya mapato katika kituo cha mabasi cha Manyoni na katika mnada pamoja na Mkuu wa Idara ya TEHAMA.
“Makusanyo hayasimamiwi vizuri, mfano katika kituo cha mabasi cha Manyoni Bw. Mussa Chacha ambaye si mtumishi ila amepewa kazi ya kukusanya mapato hayo kwa mwezi Juni alipeleka benki shilingi 1,786,000.”
“Kikundi cha wakusanya mapato walipewa PoS na mmoja wao alikusanya shilingi milioni 21.8 kwa mwezi na PoS tatu kwa muda wa miezi mitatu zilikusanya shilingi milioni 35, hawa wote lazima watoe maelezo ili hatua zichukuliwe kwa wahusika wote. Fedha hazipelekwi benki na makusanyo yanayopatikana si halisi”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Kamanda Widege afuatilie shilingi 11,021,200 zilizoingizwa Julai 12, 2022 benki kupitia namba ya malipo 992310018776 ikiwa ni makusanyo ya kituo hicho baada ya kusikia anafanya ziara katika Halmashauri hiyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanawasimamia Wakuu wa idara katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kupanga muda wa kwenda kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.
“Kila mmoja ahakikishe anatekeleza majukumu yake na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao. Manyoni hamuendi kwa wananchi, suala la usimamizi ni muhimu sana, Mkuu wa wilaya simamia hili. “Wakuu wa Idara hamuendi kwa wananchi kusikiliza kero zao, hamuendi kuwaeleza mwelekeo wa Serikali yetu.”
Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Singida inayojengwa katika kata ya Solya wilayani Manyoni na kupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa hatua iliyofikiwa. Shule hiyo ambayo itakapokamilika itapunguza utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.
Akiwa njiani kuelekea Itigi kwa ajili ya kuzungumza na watumishi wa umma, Waziri Mkuu alisimama Manyoni na kusalimia wananchi na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la machinga kutopangiwa maeneo maalumu ya kufanyia biashara zao.
Malalamiko mengine yaliyotolewa na wananchi hao ni pamoja na wajawazito kutozwa fedha pindi wanapokwenda katika hospitali ya wilaya ya Manyoni kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za afya licha ya Serikali kutoa huduma hizo za mama na mtoto bila ya malipo.
“Tufanye kazi kwa matokeo na si kwa mazoea. Eneo la usimamizi lina udhaifu mkubwa kwenye halmashauri, watu hawataki kuwasimamia wenzao na wengine hawataki kusimamiwa. Lazima uheshimu itifaki na upokee maelekezo yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwenye idara yako.”
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge alisema mkoa katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya awamu ya sita inayoongoza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mkoa umepata shilingi bilioni 252 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dkt. Mahenge alisema kuwa mbali na Mheshimiwa Rais Samia kuidhinisha mkoa huo kupata fedha hizo za miradi ya maendeleo, pia mkoa huo umepata ajira za watumishi zaidi ya 800 ambao wanawatumikia wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya na utawala.