NA ROTARY HAULE
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi ya Chalinze Modern Islamic iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wamenusurika kifo baada ya bweni la upande wa wavulana kuteketea kwa moto.
Hata hivyo,wakati bweni hilo linateketea na moto huo wanafunzi hao walikuwa katika nyumba ya ibada (msikitini) na kwamba mpaka sasa hakuna madhara yoyote juu ya wanafunzi hao na wote wapo salama.
Tukio la kuuungua kwa bweni hilo lilitokea alfajiri ya Julai 5,2022 ambapo hata hivyo chanzo cha bweni hilo kuwaka moto bado hakijajulikana.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alifika katika shule hiyo kwa ajili ya kutoa pole kwa wanafunzi hao pamoja na walimu wao sambamba na kujionea hali halisi ya tukio hilo.
"Nichukue nafasi hii kuutaarifu umma kuwa tumepata changamoto ya tukio la moto katika Shule yetu hii ya Chalinze Islamic Modern Primary School, lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu hatukupata madhara yanayohusisha athari za kifya na maisha ya wototo wetu,"amesema Kunenge.
Kunenge amesema, kwa kuwa hakuna madhara ya kiafya juu ya wanafunzi hao masomo yao yataendelea kama kawaida ambapo amewataka wazazi wa wanafunzi hao kuondoa hofu kwani hali ni shwari.
Aidha, Kunenge amesema vitu pekee vilivyoteketea ni vile vilivyokuwa vinatumiwa na wanafunzi hao ikiwemo sare, mabegi, sabuni, na baadhi ya madaftari na kwamba hakuna mwanafunzi atakayekosa masomo kwa sababu ya kukosa vifaa hivyo.
''Shule hii ni kubwa,wanafunzi ambao bweni lao limeungua moto wamepata mahali pengine pa kulala na tayari mpaka sasa wataalamu tumewaelekeza kuongea na vijana hao kwa ajili ya kuwatoa hofu na kuwashauri,"ameongeza Kunenge.
Kunenge amelishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Pwani kwa elimu wanayotoa katika shule mbalimbali kwa kuwa inasaidia kudhibiti moto pale unapotokea huku akitaka jeshi hilo kuhakikisha wanafika katika shule zote zilizopo Mkoani Pwani.
"Shule hii ilipokea mafunzo mwezi mmoja uliopita na moto huu ulipotokea vijana na jumuiya ya wafanyakazi wa shule hii walifanikiwa kuudhibiti moto huu kwa kutumia vizimia moto (Mitungi) kabla gari la zimamoto halijafika,"amesema Kunenge.
Amesema,kwa sasa tayari Serikali imeunda timu ya kitaalamu ya kuchunguza chanzo cha moto huo ili kuchukua hatua zitakazosaidia shule hiyo kuwa salama na hata Shule zingine kuziwekea mazingira mazuri ya kuepukana na majanga ya moto.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani Jenipher Shirima,amesema moto huo ulizuka mnamo alfajiri ya Julai 5 majira ya saa 11:42 .
Shirima amesema, moto huo umefanikiwa kudhibitiwa mapema kupitia vizimia moto vilivyopo shuleni hapo na kwamba kutokana na changamoto ya moto katika Shule mbalimbali Jeshi lake lipo kwenye programu ya utoaji mafunzo maalum hususani kwa Sekondari na Msingi.