NA DIRAMAKINI
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Kitivo cha Sayansi ya Kilimo na Teknolojia ya vyakula ambao wanasoma kozi ya Uchumi wa Kilimo, Maliasili na Biashara wametembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali.
Katika banda hilo la PURA wamepata kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi hiyo ikiwemo kujifunza kwa uhalisia.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao, Katibu wa Chama cha Dar es Salaam University Agribusiness and Natural Resources Economic Association, Omary Mrisho amesema lengo la kutembelea banda hilo ni kujifunza uhalisi wa kile ambacho wamekuwa wakikisoma darasani katika maisha ya kawaida.
Amesema ziara hiyo wameweza kupata elimu kwa uhalisia na kugundua ndani ya PURA kuna fursa nyingi za ajira kutokana na mfumo wa mamlaka hiyo ya serikali.
Amesema,PURA ni miongoni mwa taasisi za Serikali ambayo ina fursa nyingi za kutoa ajira nyingi kutokana na kiwango cha elimu ya mtu, ikiwa ni pamoja na wenye ujuzi wa aina mbalimbali.
“PURA ina fursa nyingi na kazi ambazo imekuwa ikizifanya ya utafutaji, uendelezaji kudhibiti na kubwa kinachohitajika ni mwamko mkubwa wa watu kuja katika maonesho haya katika banda la PURA kuja kujifunza kwani fursa zipo PURA,”amesema.
Aidha, aliwasihi wanafunzi wengine kuwa na moyo wa kutaka kujifunza kitu badala ya kukaa darasani na kusubiri pekee watoke nje ili wapate fursa ya kujifunza zaidi kwa vitendo na uhalisia wenyewe.
Naye Mkuu wa kitengo cha ushirikishwaji wazawa na uhusishaji wadau kutoka PURA, Charles Nyangi amesema Mamlaka hiyo imepata faraja na kunufaika katika maonesho hayo kwani watu mbalimbali wamepatiwa elimu juu ya majukumu yake sambamba na kuwashirikisha fursa zinazopatikana PURA.