NA SOPHIA FUNDI
WAKULIMA wilayani Karatu mkoani Arusha wametakiwa kutunza mazao yao kipindi hiki cha mavuno na kuweka akiba.
Kauli hiyo imetolewa kwenye kongamano la wakulima na Afisa Kilimo Kata ya Karatu,Flora Kanza lililoandaliwa na Kampuni ya Seed Co.
Kongamano hilo ambalo lilifanyika katika ofisi ya TFA liliambatana na onyesho la shamba darasa la mbegu mpya ya mahindi aina ya Pundamilia 555 inayotolewa na kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa bwana shamba kutoka kampuni hiyo, Rojass Kashililika amesema kuwa, mbengu hiyo aina ya Pundamilia 555 ni mbegu nzuri ambayo ina uwezo wa kutoa gunia 40 hadi45 kwa hekari moja na mkulima kutopata gharama kubwa ya kupiga dawa ya kuulia wadudu.
Alisema kuwa, mkulima akiotesha mbegu hiyo hutumia dawa mara mbili ya kuulia wadudu tofauti na mbengu zingine ambapo hutumia dawa mara tatu hadi nne hadi kuwaua wadudu.
Aliwaomba wakulima kutumia njia sahihi ya kupiga dawa ya kuua wadudu kwa kufuata njia ya kitaalam ya kupiga dawa pale mahindi yanapotimiza wiki ya tatu baada ya kuota kabla wadudu hawajaanza kushambulia ili kuweza kuwadhibiti pale watakapoanza kushambulia.
"Wakulima mnakosea sana kupiga dawa ya kuulia wadudu,mnasubiri wadudu waanze kushambulia mahindi badala ya kupiga dawa wakiwa bado hawajaanza kushambulia ili wakianza wakutane na dawa huko huko,"alisema Rojass.
Kwa upande wake Meneja wa TFA, Nathaly Kimaryo lilipo shamba darasa la mbegu hiyo alisema kuwa, lengo la kungamano hilo ni wakulima kupata uzoefu wa kilimo bora na yenye tija itakayomletea mkulima faida.