NA DIRAMAKINI
WAWAKILISHI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani wamesema kuwa, bado Watanzania wanayo nafasi ya kutumia huduma, bidhaa na mazao wanayozalisha kwa ajili ya kuyafikia masoko ya nje ambayo yanaonekana kuwa na uhitaji mkubwa.
Miongoni mwa mazao ambayo yameonekana kuwa na nafasi kubwa ni pamoja na maharage ya soya,korosho, kahawa, pamba na viungo vya vyakula ambavyo wengi wanavihitaji huko nje.
Hayo yamebaninika kupitia Mkutano Maalum wa Zoom ulioratibiwa na Watch Tanzania leo Julai 30,2022 ukiangazia juu ya Kukua kwa Diplomasia ya Uchumi na Fursa za Kiuchumi zinazopatikana nchi za Afrika ya Kaskazini, Mashariki ya Kati na Asia.
Mkutano huo ambao umerushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya mtandaoni umedhaminiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Simu za Mawasiliano ya Mkononi ya Airtel Tanzania. Wamesemaje;
MHE.MBELWA KAIRUKI, BALOZI WA TANZANIA NCHINI CHINA
"Kuna manufaa mengi yamepatikana kwenye uhusiano wetu, mfano kwenye biashara ambazo Watanzania wameuza hapa China 2019 ni zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 359, mwaka 2020 tumeuza dola za Marekani milioni 411, na mwaka 2021 tumeuza dola za Marekani milioni 601, na mwaka huu mauzo mpaka sasa yamefikia dola za Marekani milioni 230 na yataongezeka hadi kufikia dola za Marekani milioni 650 mpaka mwisho wa mwaka;
"Ubalozi wetu kwa kushirikiana Ofisi Kuu kule Guangzhou pamoja na wafanyabiashara hapa China tupo mbioni kuja na programu ya kuwasaidia Watanzania kufahamu fursa za kununua mashine mbaimbali za kuongeza thamani bidhaa zetu ambazo zina thamani kuanzia dola 300 hadi dola za Kimarekani 1000, badala ya kununua bodaboda ya milioni moja, anaweza kununua mashine ambayo ataikodisha kwa shilingi 30,000 kwa siku.
"Rai yangu kwa Wizara ya Kilimo, kuna nchi inaitwa Benin twendeni tukajifunze, mfano hapa China wanaleta Soya mara 10 ya zile ambazo Tanzania inaziuza na hata kwenye Pamba wanazalisha mara 20 ya zile tunazozalisha sisi,"amesema Balozi Kairuki.
MHE.TOGOLANI EDRISS MAYURA, BALOZI WA TANZANIA NCHINI KOREA KUSINI
"Kwa upande wa vijana Korea wanajihusisha sana kwenye Startup na tumehamasisha vijana wa Kitanzania kushiriki kwenye mashindano ya StartUp Korea, na kwenye hili tumeshirikiana zaidi na Chama cha Startups Tanzania, kwa sababu ukishinda wanakupa mtaji wa kuendeleza kampuni;
"Sisi ndiyo tulikuwa wa kwanza kuitafsiri filamu ya Royal Tour, na kwenye hilo tuliwaalika vyombo vya habari na Agencies (mawakala) wa utalii kutazama nao pamoja, na tunachokifanya hapa kila maudhui tunayoyapata tunapeleka kwenye vyombo vyao vya habari vya hapa,"amesema Balozi Mavura.
MHE.EMMANUEL J.NCHIMBI, BALOZI WA TANZANIA NCHINI MISRI
"Hapa Misri kuna soko kubwa la Korosho na bidhaa za viungo ambalo bado hatujalitumia vizuri na hii imepelekea Watanzania kutapeliwa na makampuni yasiyotambulika, rai yangu wazitumie zaidi ofisi za Balozi, sisi kuwatumikia wao kwenye hili ni wajibu wetu na tunalipwa mshahara kwa ajili ya hili;
"Baada ya Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kufanya ziara hapa Misri uwekezaji wa makampuni binafsi yanayokuja kuwekeza Tanzania imeongezeka zaidi tangu alipokuja, kampuni zaidi ya 27 zimefanya uwekezaji Tanzania wa zaidi ya dola bilioni 1. 3 ambazo zimezalishwa ajira zaidi ya 2000,"amesema.
MHE.SAID SHAIB MUSSA, BALOZI WA TANZANIA NCHINI KUWAIT
"Tumekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara waliopo Kuwait, mfano Julai 17 hadi 23 tumekutana na wafanyabiashara wanaofanya biashara ya Super Market na wameonesha nia ya kupata bidhaa za Tanzania ambazo zitaingia kwenye soko la Kuwait;
"Kuna Watanzania ambao wameajiriwa kwenye sekta ya hoteli, lakini pia kuna watanzania wameajiriwa kwenye sekta ya kuwahudumia wazee kwa ujumla Watanzania walioajiriwa Kuwait wamefikia 50,"amesema.
MHE.MEJA JENERALI JACOB GIDEON KINGU, BALOZI WA TANZANIA NCHINI ALGERIA
"Tumeanzisha ushirikiano na kampuni za Serikali za Algeria zinazojihusisha na Umeme na Gesi, Ubalozi wetu umeliungasisha shirika letu la TPDC na TANESCO ili wajenge mashirikiano na kampuni hizi ili tuweze kufaidika kama nchi;
"Algeria asilimia 80 ya dawa zinazalishwa ndani, na asilimia 20 ndiyo wanaagiza, kama Ubalozi tumeyatambua makampuni yanayozalisha dawa ili yaje kuwekeza Tanzania, ili na sisi tuwe na kiasi kikubwa cha dawa ambacho tunakizalisha kwetu,"amesema.