NA TITO MSELLEM-WM
WAZIRI wa Madini,Dkt.Doto Biteko amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la soko la madini ya Tanzanite lililopo katika Mji wa Tanzanite Mirerani uliopo wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara ambapo amemtaka mkandarasi wa zabuni hiyo kuongeza kasi ili mradi huo umalizike kwa wakati.

“Haya ni maono aliyokuwa nayo Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona mji huu unapata hadhi yake kama eneo ambalo Tanzanite inachimbwa, ukienda Geita utakuta mji huo umechangamshwa na dhahabu hivyo na Mirerani lazima inufaike na Tanzanite iliyopo katika eneo lake,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amesema Mwaka wa Fedha 2021/22 Mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini umeongezeka kufikia asilimia 44 kwenye Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 30 ya Mwaka wa Fedha 2020/21.
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole-Sendeka amempongeza Dkt. Biteko kwa kuiongoza vyema Wizara ya Madini ambapo amemshukuru kwa kuendelea kuwashirikisha wadau wa madini kutoa maoni yao ili kuandaa rasimu ya Kanuni mpya za biashara ya Tanzanite.
.jpeg)
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka nchini (CHAMMATA) Jeremiah Simon ametoa maoni yake kwa Dkt. Biteko ambapo ameshauri kwamba, Serikali iruhusu biashara ya madini ya Tanzanite yaliyoongezewa thamani ifanyike katika masoko ya madini ya hapa nchini ambapo kwa sasa Sheria ya Madini inasema biashara ya Tanzanite ifanyike Mirerani pekee.
“Madini ya Tanzanite hayaruhusiwi kutoka Mirerani kwenda kwenye masoko ya nje ya hapa, naomba zuio hili litolewe ili tuweze kuyatangaza madini yetu na pia, madini yakiongezewa thamani yaende kwenye masoko mbalimbali isiwe Mirerani pekee,” amesema Simon.