NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Nishati inapenda kuutarifu umma kwamba, kwa siku 21, kuanzia tarehe 11 hadi 31 Julai 2022, Waziri wa Nishati, January Makamba, atakuwa akitekeleza majukumu yake kutokea katika Mikoa 14 na Wilaya 38 kwa kukagua na kusimamia miradi inayotekelezwa na Wizara na taasisi za Wizara, kuzungumza na wananchi na kupokea kero, maoni na ushauri na kutoa majawabu na ufumbuzi na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati, ikiwemo vipaumbele vya Wizara kwa mwaka ujao wa fedha.
Katika awamu hii ya kwanza, mikoa itakayohusika ni Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe,Mbeya, Njombe, Ruvuma na mwisho Mtwara. Mikoa mingine itahusika katika awamu zifuatazo zitakazofanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Katika kazi hizo huko mikoani, maeneo yafuatayo yatapewa kipaumbele.
1. Upatikanaji na matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
2. Usambazaji wa umeme Vijijini na Vitongojini.
3. Upatikanaji wa umeme wa uhakika.
4. Uboreshaji wa huduma zinazotolewa na taasisi za Wizara.
5. Usambazaji wa mafuta salama na ya bei nafuu vijijini.
Lengo la jumla ni kusogeza huduma za Wizara na taasisi za Wizara kwa wananchi hasa wa vijijini na pia kuongeza uelewa kwa Watanzania kuhusu sekta ya nishati na mageuzi tunayoyafanya.
Serikali hii, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itahakikisha kwamba sekta ya nishati inachangia katika ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Wizara ya Nishati
10.7.2022