NA MATHIAS CANAL
MBUNGE wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda leo Julai 20,2022 ametembelea na kuwasalimia wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Rombo-Huruma ambayo ipo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Moshi akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni humo.

Amesema kuwa, huduma zinazotolewa na taasisi za dini ni wazi kuwa zinatolewa kwa lengo kuu la kuhudumia wananchi, lakini sio kwa ajili ya faida kama ilivyo katika taasisi zingine.

"Ndugu zangu watumishi na viongozi wa hospitali hii ya Huruma msiwe na wasiwasi juhudi za serikali zinaendelea ikiwemo kuhakikisha tunaleta huduma ya Bima ya Afya kwa wote,"amesema Prof.Mkenda.

Ameahidi kufuatilia na kutatua changamoto ya upungufu wa watoa huduma ya afya katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya kadhia ya barabara inayoenda hospitalini hapo.