NA MATHIAS CANAL-WEST
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Srikanta Pradhan ofisini kwake jijini Dar es salaam leo Julai 5, 2022.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Pradhan ameeleza kusudi la Waziri wa Elimu nchini India kumualika Waziri Mkenda kuzuru nchini humo ili kujifunza zaidi mambo yahusuyo teknolojia pamoja na uhandisi.
Waziri Mkenda amemuhakikishia Balozi huyo kuwa atafanya ziara ya kikazi nchini India mapema mwezi Agosti, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya mwanzo wa mkakati wa India kuanzisha Taasisi ya Kiteknolojia ya India nchini Tanzania itakayofundisha mambo ya Uhandisi pamoja na Teknolojia ya Mawasiliano.
Waziri Mkenda amesema kuwa, Balozi huyo amekwishakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kumueleza kusudio hilo hivyo Wizara ya Elimu itatafuta eneo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa taasisi hiyo.
Pia amesema kuwa, baada ya kutembelea nchini India atamualika Waziri wa Elimu wa India kuzuru nchini Tanzania kwa ajili ya kutembelea maeneo ambayo yatakuwa yameainishwa kwa ajili ya ujenzi ili kuwa na makubaliano ya haraka ya ujenzi.
Amesema kuwa, eneo pekee ambalo wizara imelifikiria kwa haraka ni Chuo cha Ufundi Dodoma ambacho kitakamilika Disemba, mwaka huu na kuanza udahili wa wanafunzi 1500 vilevile chuo cha TEHAMA ambacho Rais Samia ameagiza kijengwe jijini Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkenda amemueleza Balozi huyo kuwa Tanzania ingependa kuongeza mahusiano kwenye vyuo vya Ufundi ikiwemo VETA kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi.
Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania,Binaya Srikanta Pradhan amesema kuwa, Serikali ya India ingependa kwa haraka iwezekanavyo kuanzia mwakani wanafunzi waanze kuchukuliwa kwa ajili ya masomo.