NA MATHIAS CANAL-WEST
WANAFUNZI wamepata ahueni baada ya Benki ya NMB katika mwaka wa fedha 2022/2023 kutenga Bilioni 200 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9 kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.


Waziri Mkenda amesema kuwa mikopo hiyo itasaidia kupunguza idadi ya waajiriwa wanaowaombea watoto wao mikopo kwenye Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) na hivyo kutoa fursa kwa waombaji wenye uhitaji zaidi.

Ameongeza kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya kugharamia elimu ya juu ili kuendana na mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna amesema kuwa, hivi karibuni Benki hiyo ilizindua “Nuru Yangu Scholaship and Mentorship Program” kwa ajili ya kusaidia elimu nchini kwa lengo la kukata mnyororo wa umasikini na kuendeleza kizazi kijacho cha viongozi kwa kutumia njia ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Juu.

Bi.Zaipuna amesema kuwa utoaji wa mikopo hiyo ya Bilioni 200 ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa ambayo waliahidi kuanza mchakato wa kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9.