NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya Mashujaa, yatakayofanyika kitaifa Julai 25, 2022 mkoani Dodoma.
Amesema hayo leo Julai 23, 2022 baada ya kukagua maandalizi ya maadhimisho hayo, katika viwanja vya Mashujaa Mkoani Dodoma. Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na maandilizi yaliyofanywa na kamati ya maadhimisho kitaifa kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama.
“Sherehe hii itafanyika kitaifa mkoani Dodoma na itaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Viongozi wastaafu na viongozi wengine wa kitaifa.”
Waziri Mkuu amesema, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliridhia maadhimisho hayo yafanyike kitaifa mkoani Dodoma, lakini akaelekeza yafanyike nchi nzima kwa Wakuu wa Mikoa kuadhimisha siku hiyo kwa kwenda kwenye maeneo muhimu ya kumbukumbu kwenye mikoa yao.
“Kamati ya maadhimisho imefanya kazi yake vizuri sana kwa kushirikiana na vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama, eneo linafafana na tukio lenyewe, lakini maandalizi ya vikundi mbalimbali ikiwepo vyombo vya ulinzi na usalama vimeleta askari kwa ajili ya gwaride, na mwaka huu Jeshi la Uhamiaji limeanza kushiriki kikamilifu kwenye gwaride kuanzia kwenye tukio hili muhimu la mashujaa,”amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amevipongeza vyombo vya habari kwa namna ambavyo vimekuwa vikishiriki katika kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa na kwamba Serikali inathamini mchango huo.
“Serikali inawashukuru sana wananchi kwa namna ambavyo wanajitokeza katika matukio haya ya kitaifa na kujanza viwanja, tunaamini pia Julai 25 watajitokeza kwa wingi,"amesema.