Waziri Mkuu:Majukwaa ya siasa yatumike kukemea biashara, matumizi ya dawa za kulevya

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasisitiza viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao pamoja na masuala mengine ya kisiasa, wakemee biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya (wa pili kushoto) wakati alipotembelea banda la Taasisi ya Walter Reed Army Institute of Research (WRAIR) katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Mnanzi Mmoja jijini Dar es salaam, Julai 2, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ameyasema hayo leo Julai 02, 2022 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar Es Salaam. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema “Tukabiliane na Changamoto za Dawa za Kulevya kwa Ustawi wa Jamii”.

Mheshimiwa Majaliwa amesema wanasiasa hawana budi kutumia vikao na mikutano yao katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya. “Tumieni vikao vyenu vya ngazi mbalimbali pamoja na mikutano ya hadhara kuunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.”

Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini wanapotekeleza jukumu lao la kutoa mafundisho ya kiroho na kukemea dhambi na uovu pia, wawekeni msisitizo katika kukemea dawa za kulevya kwani huo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu wa aina nyingine.

Kwa upande wa wanahabari, Waziri Mkuu amewataka watumie vyombo vyao vya habari kuendelea kukemea matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Kwa upande mwingine toeni habari kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya.

“Serikali yetu inafanya mambo makubwa sana tangazeni ili Wananchi wote waweze kufahamu na kwa wale walioathirika waweze kutumia huduma zinazotolewa na hatimaye wapate tiba kamili na kuendelea kuchangia nguvu kazi ya taifa letu.”

Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika misingi ya maadili ili kuwaepusha na vitendo viovu ikiwemo matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. “Turejee kwenye asili yetu ambapo jamii nzima ilihusika katika malezi ya watoto na ilishirikiana katika kukemea maovu.”

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wote wenye taarifa muhimu kuhusu wafanyabiashara wa dawa za kulevya toeni taarifa hizo katika vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema na haraka. Wasafirishaji, wauzaji na watumiaji ni sehemu ya jamii yetu, tunao ndani ya nyumba zetu. Katika hili ninawasihi tuwe na uzalendo, tutoe taarifa, tukinyamaza tutazidi kuangamiza nguvu kazi ya taifa letu.”

“Kama nilivyosema hapo awali, suala la mapambano dhidi ya dawa za kulevya linahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu. Hivyo basi nazisihi pia asasi za kiraia pamoja na wasanii kuendelea kutoa elimu ya athari ya dawa za kulevya kwa kukemea bila kuchoka matumizi ya dawa hizi.”

Naye, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gelard Kusaya amesema dawa za kulevya ni tatizo linaloathili maendeleo ya jamii hivyo wananchi wanatakiwa kushirikiana katika kudhibiti changamoto zinazotokana na matumizi ya dawa hizo. Maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha jamii kushiriki katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

Amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo mwaka huu imetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kudhohofisha mitandao ya dawa za kulevya nchini pamoja kwa kukamata wafanyabiashara na kuteketeza dawa hizo.

“Pia, imefanikiwa kudhibiti matumizi na athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya. Kipekee nichukue nafasi hii kuvipongeza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano na kwa jitihada zao za kufanya kazi usiku na mchana bila kuchoka kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya linadhibitiwa.”

Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya waliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kupambana na kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini na kuwasihi vijana wenzao kutojiingiza katika matumizi ya dawa hizo kwa kuwa madhara yake ni makubwa ikiwa ni pamoja na kutoaminika, kutengwa na familia na jamii kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news