Yajayo Sekta ya Maji ni neema,waendelea kumtua mama ndoo kichwani

*Waziri Juma Aweso afunguka,viongozi wa wizara waonesha uzalendo wa kweli 

NA MOHAMED SAIF 

UPATIKANAJI wa huduma ya majisafi na salama ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele kikubwa na cha kipekee na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Rais Samia Suluhu Hassan akizindua mradi wa maji wa Kyaka-Bunazi wilayani Missenyi.

Aprili 22, 2022 wakati akihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Samia aliweka bayana dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya ukosefu wa huduma ya majisafi na salama. 

Mhe. Samia alisema miradi mingi imekuwa ikitekelezwa kwa kutumia fedha nyingi, lakini baada ya muda mfupi maji hayapatikani na hivyo akaelekeza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi ya maji ili kuleta tija inayokusudiwa. 

“Katika miaka hii mitano, tutaweka mkazo mkubwa katika kuimarisha usimamizi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji. Lengo letu ni kufikia azma ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijiji ifikapo mwaka 2025,” alisema Mhe. Samia. 

Azma na dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Samia ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani inatekelezwa vyema na Wizara ya Maji ambayo imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na huduma hiyo ili kutimiza ndoto ya Mhe. Rais Samia ya kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia wananchi wengi. 

Ni dhahiri kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu tangu Mhe. Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021, mafanikio mengi ya kiuchumi na kijamii yameshuhudiwa katika uongozi wake. 

Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Samia imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya maji ambapo hatua mbalimbali za maboresho zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali yake zinaanza kuzaa matunda. 

Dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuleta mageuzi katika sekta ya maji ilijidhihirisha wakati akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza ambapo alisema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye miaka mitano iliyopita, lakini tatizo la maji bado lipo kwenye maeneo mengi nchini. 

Mhe. Rais Samia alibainisha mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya maji miaka iliyopita, na kusema kuwa anatambua upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama bado ni changamoto kwenye maeneo mengi na kwamba kuna hitaji usimamizi imara kwenye miradi ya maji. 

Kauli ya Mhe. Rais Samia sio tu kwamba inadhihirisha kuwa safari iliyopigwa ni ndefu, lakini bado inaendelea na mafanikio na matarajio ni makubwa. Wizara ya Maji imepewa dhamana ya kuhakikisha mabadiliko yenye tija yanafanyika ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi na wadau wote. 

Kiongozi mkuu wa nchi ameainisha vyema nini anachotarajia kuona kwenye Sekta ya Maji, swali la kujiuliza ni je azma na dhamira yake ya kumtua mwanamke ndoo kichwani inatekelezeka kama anavyotarajia? Wizara ya Maji imemuelewa kwa kiasi gani katika hili na hali ikoje ikilinganishwa na hapo kabla? 

Majawabu ya maswali haya yapo wazi na yanajidhihirisha kila kukicha. Wananchi kwenye maeneo mbalimbali wanaendelea kushuhudia jitihada zinazofanywa na Serikali yao kwani maeneo mengi hivi sasa yanapata neema ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wote, na kazi hiyo inazidi kushika kasi. 

Hivi karibuni, wakati anazindua mradi wa majisafi wa Kyaka-Bunazi wilayani Missenyi mkoani Kagera, Mhe. Rais Samia ameonyesha dhahiri kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya Maji kwa kuifikia azma yake ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. 

Mhe. Rais Samia anasema: “hatimaye adha ya ukosefu wa maji iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa Kata za Kyaka na Kasambya Wilayani Missenyi imepata ufumbuzi kwa kujengewa mradi mkubwa wa shilingi bilioni 15.7 ni mradi utakaonufaisha watu wapatao 65,470.” 

Anaweka bayana namna ambavyo Wizara ya Maji imeielewa dhamira yake ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani na anaipongeza kwa namna inavyotekeleza maelekezo na maagizo ya Serikali. 

“Wizara ya Maji kwa mara nyingine tena mmenifungua uso Mama yenu, juzi nilisema Wizara ya maji mnafanya mambo mazuri na leo kwa mara nyingine tena mmenikosha Mama yenu asanteni sana,” anasema Mhe. Rais Samia mbele ya umati uliokusanyika kushuhudia uzinduzi wa mradi huo eneo la Kyaka. 

Ni dhahiri shahiri kuwa pongezi hizo za Mhe. Rais Samia kwa Wizara ya Maji ni kwamba yajayo yanafurahisha, majawabu ya maswali haya yamepatikana; kumbe upatikanaji wa majisafi na salama kwa wote inawezekana na hakika mwanga wa kutufikisha huko umedhihirika. 

Majawabu ya maswali haya pia tunayapata kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bi. Zuhura Yunus wakati anazungumzia mafaniko ya mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, mwezi Machi, mwaka huu, ambapo anatubainishia uhalisia wa mambo yanavyokwenda na hatua zilizopigwa hadi sasa. 

Bi. Yunus anafafanua kwamba hadi mwezi Machi, 2022 jumla ya miradi 463 ya maji imekamilika ambapo miradi 412 ikiwa ni miradi ya vijijini na 51 ya mijini. 

“Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya miradi minne imekamilika kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambayo ni mradi wa Mkuranga, mradi wa maji Mboga-Chalinze, mradi wa maji Kisarawe-Pugu-Gongolamboto na mradi wa maji Bwawa-Mlandizi,” anafafanua Bi. Yunus. 

Bi. Yunus anabainisha mafanikio hayo kwa mikoa mingine na anaitaja miradi hiyo kuwa ni Nyamtukuza-Nyangh’wale-Geita, mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji katika Manispaa ya Bukoba, miradi ya Misungwi, Magu, Lamadi, mradi wa Ntomoko-Kondoa-Chemba na mradi wa Jijini Dodoma uliohusisha uchimbaji wa visima vitatu na kuongeza uzalishaji maji jijini humo. 

Akizungumzia utendaji wa wizara anayoisimamia na mafanikio yaliyopatikana kwenye uongozi wa Mhe. Rais Samia, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa Mkoani Arusha, mwezi Machi, 2022, anasema anasimamia maelekezo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama na yenye kutosheleza. 

“Mhe. Rais ametupa Wizara ya Maji maelekezo mahsusi wakati anahutubia Bunge ambapo alinisimamisha kama Waziri wa Maji na kunipa maelekezo; anasema yeye ni Mama hataki kusikia, hataki kuona Watanzania waishio vijijini na mijini wanateseka kwa suala zima la maji,” anasema Waziri Aweso. 

Waziri Aweso anasema Mhe. Rais Samia hataki kusikia wala kuona ucheleweshwaji wa ukamilishwaji wa miradi ya maji; hataki kusikia wala kuona ubadhirifu kwenye miradi ya maji na hataki kusikia wala kuona wakandarasi wababaishaji wasiokuwa na uwezo wakipewa kazi za ujenzi wa miradi ya maji. 

“Baada ya maelekezo haya ya Mheshimiwa Rais Samia, nilikaa na timu nzima ya Wizara ya Maji na kuelekeza twende ‘site’ kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza,” anasema Mhe. Aweso. 
Muonekano wa mradi wa maji wa Kyaka-Bunazi. 

Waziri Aweso anasema utekelezaji wa miradi ya maji unategemea upatikanaji wa fedha na anamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuipatia fedha kwa wakati Wizara ya Maji ili kutekeleza azma ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.

“Ninamshukuru Mhe. Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutusapoti kwani tunapata fedha kwa wakati. Kwenye bajeti tulitengewa bilioni 646 fedha za maendeleo na hadi Januari, 2022 tumepokea zaidi ya bilioni 480 ambayo ni zaidi ya asilimia 74,” anasema Waziri Aweso. 

Anasema awali, Wizara ya Maji ilikuwa ikipokea chini ya asilimia 50 ya fedha za maendeleo, lakini hadi kufikia Januari, 2022, Wizara imekwishapokea zaidi ya asilimia 74 fedha ambazo zimesaidia kukamilisha miradi 463. 

“Mhe. Samia ni Rais wa kusema na kutenda, amenielekeza pamoja na kutoa fedha, lakini atakuwa mstari wa mbele kusimamia na kufuatilia. Ameonyesha dhamira yake waziwazi ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani, kila pande ya Tanzania tunamradi unaendelea,” anasema Waziri Aweso. 

Anataja baadhi ya miradi iliyokamilika na ambayo inaendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini na anabainisha kwamba Wizara ya Maji imepokea shilingi bilioni 139 ambazo zinakwenda kutekeleza miradi 218 katika kila jimbo na pia kupitia fedha hizo mitambo 25 ya kuchimba visima inanunuliwa na hivyo kufanya kila mkoa kuwa na mtambo wake. 

Waziri Aweso anasema katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Mhe. Rais Samia, Wizara imepokea kiasi cha shilingi bilioni 41 ambazo ni maalum kwa ajili ya kulipa wakandarasi waliokuwa wakidai fedha baada ya kukamilisha shughuli walizopewa na Wizara kwa ajili ya ujenzi wa miradi. 

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Aweso na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bi. Zuhura Yunus ni dhahiri kwamba yajayo yanafurahisha, watendaji wa Wizara ya Maji wametambua vyema nini Mhe. Rais Samia anataka na nini anatarajia kutoka kwao. 

Kwa utekelezaji huo wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Maji chini ya uongozi wa Waziri Jumaa Aweso (Mb) kwa ushirikiano wa karibu na wasaidizi wake akiwemo Naibu Waziri, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba na Menejimenti nzima ni kwamba Sekta ya Maji sasa imepata mwarobaini. 

Hakuna ubishi katika muhula huu wa kwanza wa uongozi wake, Rais Samia ameonyesha kasi na vitendo kwenye ujenzi wa miradi ya maji. Mambo yanakwenda bila kikwazo kwa wananchi kupata huduma ya maji. Tunasema Kazi iendelee… Jiandae kuhesabiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news