NA DIRAMAKINI
VIJANA nchini wameombwa kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022 kwa kujitokeza kuhesabiwa ili kuiwezesha Serikali kuwajumuisha katika mipango ya maendeleo kulingana na idadi yao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Vijana wa Chama cha Alliance for Change and Transparency-Wazalendo ( ACT- Wazalendo), Abdul Nondo alipozungumza na wanachama na wapenzi wa chama hicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana duniani ambayo chama hicho kitaifa kiliadhimisha katika Mkoa wa Lindi.
Akieleza sababu ya kuadhimisha katika mkoa wa Lindi, Nondo alisema vijana wa chama hicho wanatambua kwamba changamoto zinazowakabili vijana wa Lindi zinashabihiana na changamoto za vijana wengine nchini.
Nondo alisema ACT- Wazalendo kupitia ngome yake ya vijana kinaamini katika nguvu za vijana katika kuchagiza maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwani vijana ni kundi lenye idadi kubwa ya watu nchini.
Alisema, ingawa kundi la vijana ni kubwa kwa idadi ya watu lakini ni kundi kubwa lililosahaulika. Huku akisema Serikali inatumia takwimu za Sensa ya mwaka 2012 ambayo kwa sasa imepita miaka 10.
"Kitakwimu, Serikali hutumia takwimu za Sensa ya 2012, miaka kumi iliyopita inayosema idadi ya watu Tanzania ni milioni 44.9, asilimia 35. Hizi ni takwimu zisizo na uhalisia kwani ni miaka kumi sasa imepita, idadi ya watu imeongezeka sana,hivyo ili pawepo takwimu sahihi ambazo zitaipa dira Serikali ni vema vijana tukajitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya mwaka huu,"alisema.
Kwakuzingatia ukweli huo Nondo alitoa wito kwa vijana wajitokeze kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi huu wa Agosti, tarehe 23, mwaka huu wa 2022 ili serikali ipate idadi sahihi ya watu. Wakiwemo vijana badala ya kutumia sensa ya mwaka 2022.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya sasa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 60. Ambapo asilimia 70 ya idadi hiyo ni vijana. Ambao wana umri wa kuanzia miaka 18 hadi 40.