NA DIRAMAKINI
UONGOZI wa Azam FC ya jijini Dar es Salaam umeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika kukiweka sawa kikosi cha timu hicho ambacho kinashiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kuwa bora.

Ni uwekezaji ambao unaimarisha mikakati ya awali ikizingatiwa tayari walishawekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwanja wa kisasa uliopo Kata ya Chamanzi Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mbali na wachezaji wakiwemo wakufunzi waliobobea katika timu hiyo, leo Agosti 20, 2022 uongozi huo umempokea mtaalamu wa tiba za wanamichezo, Joao Rodrigues kutoka Ureno ambaye anaingia kandarasi timu hiyo.
Rodrigues ni mtaalamu wa viwango mwenye viwango vya juu kwenye tiba za wachezaji ambapo aliwahi kufanya kazi na mabingwa wa Ureno, FC Porto.

Haya yanajiri ikiwa awali Mkurugenzi wa Azam FC, Yusuf Bakhresa kabla ya kuanza msimu huu aliahidi atawapa furaha mashabiki wa timu hiyo kwa kuleta wachezaji wa hali ya juu, kocha wa viungo, kocha wa makipa na mahitaji mengine ya msingi ili kukifanya kikosi hicho kuwa bora zaidi.