NA MWANDISHI WETU
IMEELEZWA kuwa, yapo matumaini kwamba mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yakasomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Septemba, mwaka huu.
Ni kauli ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia wito wa serikali kukutana na wadau wa habari nchini.
Hivi karibuni, serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeitisha mkutano wa wadau wa habari kuzungumzia vipengele mbalimbali vya habari vinavyoonekana kuminya tasnia hiyo.
Mkutano huo umepangwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 11 hadi 12, mwaka huu, katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Mchakato umeanza kuzaa matunda, wiki hii tumepata mwaliko kutoka serikalini ambapo tutakuwa na mkutano wa pamoja kati ya serikali na wadau wa habari utakaofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere.
“Mjadala huo unahusu kujadili vifungu vya sheria za habari ili kuona jinsi gani tunarekebisha kifungu kwa kifungu, ili ziwe nzuri kama tulivyokuwa tukiomba siku zote,” amesema.
Amesema, mchakato wa mabadiliko umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza na kwamba, hatua ya serikali kuitisha mkutano wa wadau kujadili vipengele vya sheria hizo, unaashiria kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwasilishwa kwenye Bunge la Septemba mwaka huu.
“Kuna mwelekeo sasa kwamba, kama tunakwenda kwenye huu mkutano wa tarehe 11 na 12 Agosti mwaka huu, tunaweza kuona hii sheria inapelekwa bungeni kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza.
“Sasa tusiende kusoma sheria ambayo kwamba tutaenda na mivutano, tumeshakubaliana na Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), tumeishakubaliana na Mheshimiwa Rais (Rais Samia Suluhu Hassan), kwa hiyo tunaamini kwamba, watatusikiliza kwenye mkutano na tutalizungumza ili tupitie yote ili tusipeleke vipande vipande,"amesema.
Balile amesema, kwenye mapendekezo yao miongoni mwa vipengele wanavyoyaka kufanyiwa kazi ili kulinda uhuru wa habari ni pamoja na kuondoa utitiri wa vyombo vinavyosimamia tasnia ya habari.
Na kwamba, muundo wa vyombo vilivyoelekezwa na sheria iliyopo, unaweza kuvunjwa na kuunda chombo kimoja ambacho kitakuwa imara na kusimamiwa kisheria kama ilivyo katika taaluma nyingine nchini.
“Sisi hatupingi Bodi ya Ithibati ila tunasema kwamba, kutenga Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Vyombo vya Habari, unakuwa umeleta shida kwa sababu, ukiwa na Baraza la Ithibati halafu Baraza Huru la Habari, unakuwa na vyombo viwili vinavyofanya kazi ile ile.
“Lakini tunasema, kama wanasheria wanayo Tanganyika Laws Society. Hiyo hiyo inafanya kazi ya ithibati (inawapa vitambulisho), inasuluhisha pale mwanasheria anapokwenda kinyume. Hivyo, tunataka chombo kimoja (Baraza la Habari) litakaloundwa kwa mujibu wa sheria liwe na mamlaka yote hayo.
“Baraza tunalotaka litakuwa na kazi ya kufanya ithibati; kwamba litawapa waandishi vitambuliisho, litashughulikia kesi zinazohusu tasnia ya habari lakini kama ilivyo sasa,”amefafanua.
Balile amehoji, ikiwa taaluma nyingine kama madaktari, wagavi pia mainjinia wamekuwa na bodi zao ambazo zinashughulikia kila kitu kinachowahusu, lakini kwenye tasnia ya habari igawanywe vipande vipande.
“Katika tasnia ya habari imegawanywa vipande vinne, imegawanywa kwenye Baraza Huru la Vyombo vya Habari, imegawanywa kwenye Baraza la Ithibati, imegawanywa kwenye Mfuko wa Mafunzo na imegawanywa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.
“Sisi tunasema, hatuna shida na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, anaweza kuendelea kuwepo na akafanya shughuli zake ambazo zimeanishwa chini ya sheria, lakini hivi viwili; Mfuko wa Mafunzo na Baraza la Ithibati viunganishwe kwenye Baraza Huru la Vyombo vya Habari.
“Labda watueleze kama wanamaslahi ya ziada, kwa nini wanataka waendelee na mfumo huu ambao ni wa serikali kuthibiti vyombo vya habari? Basi watueleze, tutaelewani pengine,”amesema.